Kichuya aikomalia Yanga tu

Muktasari:

Winga huyo aliyepo timu ya taifa, Taifa Stars, ambayo kesho Jumamosi itashuka Uwanja wa Amahoro mjini Kigali kucheza mechi ya marudiano ya kufuzu fainali za Chan 2018 dhidi ya wenyeji Rwanda, alisema Yanga haimpi shida kwa vile anajiamini.

MASHABIKI na wachezaji wa Yanga, huenda bado wanaendelea kumuota Shiza Kichuya kwa jinsi mabao yake mawili yalivyowakata maini katika mechi ya watani msimu uliopita, lakini kama wanadhani watapumua, wamsikie anachokisema.

Kichuya aliyesajiliwa Simba kutoka Mtibwa Sugar, ndiye aliyefunga bao la kusawazisha katika mechi iliyojaa utata ya Oktoba Mosi, 2016 kabla ya kufunga bao la ushindi mechi ya marudiano na kuwazima kabisa Yanga, alisema yupo tayari kufanya yake.

Winga huyo aliyepo timu ya taifa, Taifa Stars, ambayo kesho Jumamosi itashuka Uwanja wa Amahoro mjini Kigali kucheza mechi ya marudiano ya kufuzu fainali za Chan 2018 dhidi ya wenyeji Rwanda, alisema Yanga haimpi shida kwa vile anajiamini.

Kichuya alisema anafahamu Yanga watakuwa wakimpangia mikakati kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 23, sambamba na ile ya Ligi Kuu Bara Oktoba 14, lakini anaendelea kujiweka sawa ili kuisaidia timu yake.

MSIKIENI MWENYEWE

Kichuya alisema kuwepo kwake Stars kumemsaidia kumweka sawa kabla hata hajavaana na Yanga na kwamba wapinzani wao wajiandae tu kupata maumivu kwa sababu yupo Simba kwa ajili ya kuipa mafanikio.

“Sipendi kuwa mwongeaji sana, ila napenda kufanya sana kazi uwanjani, naendelea kujipanga kulinda heshima yangu, hata kama sitafunga lakini lazima nitoe pasi ya bao ili kuibeba Simba timu inayonifanya niishi mjini,” alisema Kichuya.

Alisema mechi za Kombe la Cosafa na zile za Chan zimesaidia kumpa uzoefu zaidi kwani amekutana na nyota mbalimbali wa kimataifa, hivyo Yanga kama watakaa vibaya wasishangae wakapigwa nyingi Taifa.

JEZI YA OKWI

Kichuya alizungumzia ujio wa Emmanuel Okwi ndani ya kikosi chao na kusema kwamba ni faraja kwao, lakini kuhusu jezi aliyokuwa akiitumia yenye namba 25, alisema atamuachia Mganda huyo kwa sababu hajawahi kuamini katika namba ya jezi.

“Siamini katika jezi, hata nikivaa ya kipa ni sawa kwa sababu kwangu kiwango cha uwanjani ndio kila kitu na sio namba ya jezi, hivyo nitamuachia Okwi kama ataitaka kwani alishaizoea kuitumia siku za nyuma alipokuwa hapa,” alisema.

“Kwangu Okwi ni somo, lazima nijue kwa nini jina lake limekuwa kubwa licha ya kwamba hakuwepo, kila mara anatamkwa kuanzia kwa mashabiki na viongozi, simchukulii poa, nafurahia kucheza naye ili nipige hatua zaidi kisoka,” alisema.

MAWEJJE AGOMA

Katika hatua nyingine straika Tony Mawejje ameugomea uongozi wa Simba uliotaka kumsainisha mkataba wa miaka miwili kwa dau la Dola 30,000 na badala yake alitaka dau hilo lifanywe kwa mkataba wa mwaka mmoja tu.

Taarifa za ndani zisizo na shaka zinasema kuwa Mganda huyo aliamua kukomaa asaini mkataba huo mfupi kwa kiasi hicho cha fedha, lakini mabosi wa Simba nao wakamkazia, hivyo kukwamisha mipango ya mkali huyo kutua Msimbazi.

“Dili la Mawejje limeshindikana, baada ya kushindwana kwenye dau, Simba ilitaka asaini mkataba wa miaka miwili kwa kiasi cha dola 30,000 lakini yeye aligoma na kutaka mkataba wa mwaka mmoja na Simba wakamgomea,” kilisema chanzo makini ndani ya Simba.

Simba iliyopo Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya ndani na ya kimataifa ilimtaka Mawejje kuiongezea makali eneo lake la mbele hasa kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.