Kichuya, Chilunda mchongo mkali

MTANZANIA, Emily Mgeta anayecheza soka la kulipwa nchini Ujerumani amewapa dili nyota wanaofanya vizuri Ligi Kuu akiwemo staa wa Simba, Shiza Kichuya na Shaaban Iddy Chilunda wa Azam FC, kuachana na soka la bongo na kwenda Ulaya.

Mgeta anayechezea timu ya VfB Eppingen ya Daraja la Tano nchini humo, alisema Kichuya na Chilunda wasiogope namna ya kuanza maisha mapya nje ya Bongo, akiwasisitiza miguu yao itawafanya wawe mamilionea watakaoheshimika baadaye.

Alisema sababu zinazowanyima fursa nyota wengi wa Tanzania kuwa ni mazingira na elimu ambayo ingewasaidia kujua wao ni kina nani katika ulimwengu wa sasa.

“Wachezaji wa Tanzania wamezoea wanapoonana na kiongozi mara amepewa Shilingi 20,000, mara shabiki kampa hiki na kuona maisha wameyapatia, niwaambie ukweli wanazikalia pesa kuliko wanazopata kwa sasa.

“Hata kama nacheza ligi ya Daraja la Tano, nikirejea Tanzania nitakuwa bora zaidi ya huyo anayecheza Ligi Kuu, kila kitu kinawezekana kwa sasa mimi nina uwezo wa kuzungumza lugha nyingi kama Kifaransa, Kijerumani na Kiingereza, lakini hapo awali nilikuwa naona kama miujiza hivyo ni vema wakaiga mfano kwangu hasa kwa wale ambao walicheza na mimi,” alisema.