Kiberenge Yanga kazi anayo

MAWINGA Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi ni kama wamemchongea Kiberenge mpya wa Yanga, Baruani Yahya, anayetajwa kuwa mrithi wa Simon Msuva Jangwani.

Mwashiuya na Mahadhi walisajiliwa na Yanga kwa matumaini makubwa wakitokea Kimondo na Coastal Union mtawalia, lakini hawakufiki kiwango cha juu, jambo linalompa mtihani Yahya atakayecheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo Yahya ambaye amesaini Yanga wiki iliyopita, aliliambia Mwanaspoti kuwa ni nafasi nzuri ambayo ameipata kujiunga na timu hiyo lakini amewaomba mashabiki wawe naye bega kwa bega.

“Natambua wengi wanahitaji kucheza katika klabu kama hii. Kikubwa nitajitahidi kufanya mazuri nikiwa hapa lakini pia mashabiki wanatakiwa kuwa bega kwa bega na klabu,” alisema.