Kiatu cha Samatta ni timu nzima unaambiwa

Muktasari:

“Kiatu hiki nilinunua Euro 240 (Tsh 570,000),” alijibu, Samatta na kuhoji huku akicheka: “Sasa kwa nini umeniuliza swali hilo.”

HIVI unajua kiatu anachovaa straika, Mbwana Samatta ‘champion boy’ kinaweza kununua viatu vya maana vya timu nzima ya Mwadui au kikamlipia pango ya chumba kwa muda wa mwaka mzima, mchezaji wa Kibongo.

Samatta anayekipiga klabu ya Genk ya Ubelgiji alinaswa na Mwanaspoti Uwanja wa Taifa akifanya mazoezi na kiatu alichonunua kwa gharama ya Euro 240 sawa na Sh. 570,000  za kitanzania kutoka kampuni ya Nike.

Straika huyo ambaye anafanya vizuri Ulaya akiwa na klabu yake hiyo na alitajwa kwenye kikosi bora cha Europa cha mwezi uliopita huku akitamka kwa mdomo wake gharama yake akiwa amekishika mkononi.

“Kiatu hiki nilinunua Euro 240 (Tsh 570,000),” alijibu, Samatta na kuhoji huku akicheka: “Sasa kwa nini umeniuliza swali hilo.”

Lakini ukweli wa mambo,  kiasi cha pesa hiyo kinaweza kuwanunulia viatu wachezaji 11 sawa wa timu moja kama Mwadui, Tanzania Prisons na nyingine ambao sehemu yao kubwa hununua viatu kwa gharama ya shilingi elfu 40, 50, 60 na ikizidi sana inakwenda hadi laki moja.

Pia, kulingana na maisha ya vijana wengi pamoja na wachezaji wa Kitanzania wanaoishi maisha ya kupanga vyumba jijini Dar es Salaam ambapo chenye ubora gharama yake inaweza kuwa kati ya elfu 40, 50, 60 na kuendelea. Hivyo shilingi laki tano na elfu sabini iliyonunua kiatu cha Samatta, inaweza ikamlipia kodi ya mwaka mzima.

SAID HATAMSAHAU

Basi bwana wakiwa katika mazoezi yao ya kawaida ya kikosi cha Taifa Stars, Samatta na wachezaji wengine walikuwa wakijifua na kukatengenezwa kizuizi ambacho washambuliaji walitakiwa kufunga na aliyekaa golini alikuwa, Said Mohammed.

Sasa wakati Samatta anakwenda kushambulia, alimpiga Said  chenga ya mwili hatari, iliyomfanya adondoke chini bila kutegemea. Kitendo hicho kilishuhudiwa na sehemu kubwa ya watu waliokuwa wanafuatilia mazoezi hayo, kikawafanya waishiwe nguvu kwa cheko, lakini Said naye alijikuta akitumia takribani dakika mbili chini akijitathmini.