Kessy akutana na ‘sapraizi’ Yanga

Muktasari:

Kessy aliyenyakuliwa kitatanishi toka Simba, alisema ujio wa nyota wapya Yanga umeongeza presha kikosini, lakini hiyo ni dalili njema za Yanga kutisha msimu huu.

BEKI wa Yanga, Hassan Kessy, ametamka kauli ya kishujaa kwamba mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 23 kati yao na Simba ni nyepesi sana, ila kinacholeta presha ni sapraizi ya majina makubwa ya mastaa waliosajili kikosini.

Kessy aliyenyakuliwa kitatanishi toka Simba, alisema ujio wa nyota wapya Yanga umeongeza presha kikosini, lakini hiyo ni dalili njema za Yanga kutisha msimu huu.

“Kuna tofauti ya ugumu wa mechi na majina makubwa ya wachezaji, mfano mzuri ni uhamisho wa Ibrahim Ajibu kutoka Simba kuja Yanga, hilo linaibua presha kwa mashabiki kuona kama kuna kitu cha ajabu kinakuja wakati soka ni lile lile,” alisema Kessy.

Kuhusu mechi hiyo ya Ngao ya Jamii, alisema haoni cha ajabu katika mechi hiyo zaidi ya mchezaji kuzingatia majukumu yake uwanjani na kutovunja sheria za soka kwa maana ya mashabiki kupata burudani inayotakiwa.

“Mtu kama Emmanuel Okwi ni mchezaji gani asiyemjua mpaka akaleta presha kwenye mechi hiyo bwana? Binafsi nimejipanga kwa majukumu ya siku hiyo kama ilivyo kwenye mechi nyingine zinazotakiwa niwajibike ili timu ishinde,” alisema.

Kessy alisema amegundua ndani ya Yanga viongozi wanawajali na kuthamini wachezaji jambo linalochangia kujituma kwao uwanjani na kuwapa morali tofauti na alipotokea.

“Nimegundua kwa nini Yanga wanakuwa na mafanikio, viongozi wapo karibu na wachezaji wakiwatia moyo, unajua mchezaji anapodharauliwa hukata tamaa na kushindwa kujituma uwanjani,” alisema bila kufafanua kwa undani.