Kesi ya vigogo Simba yafikia patamu

Muktasari:

  • Juni 12, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilitoa muda wa siku 10 kwa upande huo wa mashtaka kurekebisho hati ya mashtaka, kwa kumtoa mshtakiwa wa tatu na wanne, ili kesi ya msingi iendelee.

MAMBO yameiva. Upande wa Mashtaka katika kesi ya kula njama na kughushi inayowakabili vigogo wa Simba, akiwemo Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, umeieleza mahakama wapo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa amri ya mahakama waliyopewa.

Juni 12, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilitoa muda wa siku 10 kwa upande huo wa mashtaka kurekebisho hati ya mashtaka, kwa kumtoa mshtakiwa wa tatu na wanne, ili kesi ya msingi iendelee.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai alisema Alhamisi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

“Tupo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa amri tuliyopewa na mahakama hii, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” alidai Swai.

Awali, Wakili wa Aveva, Evodius Mtawala aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha kwa wakati amri waliyopewa na mahakama ili kesi iweze kuendelea.

“Tulijua leo (Jana) upande wa mashtaka watakuwa wamekamilisha amri waliyopewa na mahakama kwani ni mwaka sasa wateja wetu wanaendelea kusota mahabusu.”

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba uliutaka upande wa mashtaka kukamilisha haraka amri waliyopewa na mahakama ili hatua nyingine ziweze kufanyika.

“Upande wa mashtaka, nawapa hadi Julai 5, mwaka huu mkamilishe utekelezaji wa amri ya mahakama mliyopewa mje na maelezo yasiyo na visingizio” alisema hakimu.

Kesi hiyo inayowakabili kina Aveva na wenzao wawili akiwamo Mwenyekiti wa Usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao hawajakamatwa imeahirishwa hadi Julai 5.