Kesi ya Wema ngoma bado

Wema Sepetu (kushoto) akiwa na Meneja wake, Martin Kadinda nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. 

KESI inayomkabili, Wema Sepetu bado mbichi. Hii ni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana Jumatano kukwama kutoa uamuzi wa kupokea au kutopokea kielelezo cha hati ya ukamataji mali, nyumbani kwa Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006.

Hatua hiyo imetokana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kutomaliza kuandaa uamuzi, hivyo kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Nyota huyo wa filamu nchini na wenzake wawili, wanakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ilipangwa kutolewa uamuzi jana katika mahakama hiyo, baada ya Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala kupinga hati hiyo kutolewa kama kielelezo mahakamani hapo kwa madai hakijakidhi vigezo vya kisheria.

Mbali na Wema, washtakiwa wengine ni Angelina Msigwa na Matrida Seleman Abbas.

Ilidaiwa kuwa Februari 4, 2017 katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio, washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.