Kenya yapanda viwango, ikiukosa ubingwa wa Kombe la Dunia Raga

Nairobi. Ndoto ya Kenya ya kutaka kulipa kisasi dhidi ya mahasimu wao, Fiji 7s imezimika baada ya kukubali kichapo kikali cha 22-5 kwenye mchezo wa fainali ya msururu wa saba wa Kombe la Dunia la Raga, Hong Kong 7s  uliochezwa leo Jumapili, huku ikipanda kwenye viwango vya dunia katika mchezo huo.
Hii ni mara ya pili Kenya inakubali kichapo kutoka kwa Fiji 7s msimu huu kwani itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, katika fainali ya msururu wa Vancouver 7s, iliyofanyika nchini Canada, Kenya ilitandikwa 31-12.
Dalili za kuzama kwa jahazi la Shujaa zilionekana mapema baada ya Collins Injera na Willy Ambaka kulimwa kadi za njano na hivyo Shujaa 7s kulazimika kucheza uwanjani wakiwa pungufu.
Hali hiyo iliipa Fiji 7s, mwanya wa kuiangamiza Kenya ambapo walijiandikia 'tries' za haraka muuaji akiwa ni Amenoni Nasilasila. hadi kipindi cha kwanza kinamalizika walikuwa wanaongoza 17-0.
Kipindi cha pili vijana wa Innocent Simiyu walizinduka na kuishambulia ngome ya Fiji, juhudi zilizoleta matunda ya try mbili, wafungaji wakiwa ni Billy Odhiambo na Oscar Ouma. Juhudi hizi hata hivyo, hazikubadili hatma ya Kenya na Fiji wakaibuka mabingwa kwa ushindi wa 24-12.
Kenya ilitinga fainali kwa kuisulubu New Zealand (21-12) katika mchezo wa Nusu fainali ya kwanza huku Fiji ambao kwa sasa wanajivunia ubingwa wa Vancouver na Hong Kong waliingia fainali kwa kuilaza Afrika Kusini kwenye mechi ya nusu fainali ya pili.

Kenya yaongeza pointi 19
Licha ya kufungwa kwenye fainali, habari njema kwa mashabiki wa mchezo wa raga nchini ni kwamba, Shujaa imeongeza alama 19 katika kapu lake na hivyo kuwafanya wafikishe alama 83 za jumla katika misururu yote ya Kombe  la Dunia la Raga, maarufu kama HSBC World Rugby Sevens Series.

Innocent Simiyu sasa freshi
Wakati huohuo, matokeo ya Vancouver 7s na Hong Kong 7s yameendelea kusafisha nyota ya kocha wa Shujaa 7s, Innocent Simiyu na sasa ana kila sababu ya kupata usingizi.
Ishu iko hivi, kabla ya Vancouver 7s na Hong Kong 7s, wadau wa mchezo wa raga nchini, walionesha kupoteza matumaini na Kocha huyo kufuatia Shujaa kushindwa kuandikisha matokeo mazuri tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa Shujaa 7s.
Wadau wengi, walihoji uwezo wa Simiyu huku wengi wakishiniza kocha wa zamani wa Shujaa, Benjamin Ayimba arudishiwe chama lake. Furaha ya Simiyu inatokana na rekodi mpya aliyoweka ya kuwa kocha wa kwanza katika historia ya mchezo huo nchini, kutinga fainali mbili mfululizo ndani ya msimu mmoja.