Kenya yaanza kwa kishindo London 7s

Saturday June 2 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Timu ya taifa ya mchezo wa Raga ya Kenya, Shujaa 7s, imeanza vyema kampeni katika mashindano ya London 7s yanayooendelea kwenye Uwanja wa Twickenham, Jijini London, England.

Kenya ilianza kwa kuwalazimisha Marekani vinara wa Kundi C, sare ya 19-19 katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa majira ya saa 7:42 mchana kabla ya kuishushia kipigo cha 24-21 taifa la Ufaransa.

Marekani wamejihakikishia uongozi wa kundi wakiwa na alama 5 sawa na Kenya, lakini wanawazidi kwa idadi ya mabao. Hii ni baada ya kuitandika England mabao 31-14.

Wenyeji wa msururu huu, England wanashika nafasi ya tatu, kutokana na ushindi wa 34-0 walioupata dhidi ya vibonde wa kundi Ufaransa.

Kwa mujibu wa ratiba, mchezo wa tatu wa kundi C, utapigwa baadae ambapo Kenya itakutana na England huku Marekani wakimaliza udhia dhidi ya Ufaransa.