Kayuni, msola wafichua siri za kocha

Muktasari:

Mbelgiji huyo ni kocha wa aina yake kwani alifanyiwa usajili na jopo la wataalamu wanne na kumpitisha kuwa anafaa kuwaongoza Wekundu wa Msimbazi mwanzo mwisho.

KWA kumnasa kocha, Patrick Aussems, mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba SC, wametajwa kuzivamia anga za vigogo wengine wa soka la Afrika.

Mbelgiji huyo ni kocha wa aina yake kwani alifanyiwa usajili na jopo la wataalamu wanne na kumpitisha kuwa anafaa kuwaongoza Wekundu wa Msimbazi mwanzo mwisho.

Jopo hilo liliongozwa na Mkufunzi wa FIFA, Sunday Kayuni, Salum Madadi (aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania), Dk. Mshindo Msolla (Kocha wa zamani wa Taifa Stars) na Oscar Mirambo (Kocha wa timu ya taifa ya vijana), ambao wamesema Aussems ni bonge la kocha na Simba wamelamba dume la mbegu.

Wakizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa, baadhi ya wataalamu hao waliomfanyia usaili kocha huyo, wamesema Mbelgiji huyo ni mtu sahihi wa kuivusha Simba ambayo ina matarajio makubwa kwa sasa.

Wamesema kuwa wameiangalia taaluma yake, mahali alikofundisha, uzoefu, ufundi, matarajio ya Simba, mazingira ya ligi ya Tanzania na mambo mengine muhimu.

“Walikuwepo makocha wengi waliotaka kazi Simba, lakini huyo ndiye alikuwa chaguo sahihi, tulipitia mambo mengi ambayo tuliyatumia kumsaili, vigezo vyote alitimiza ndiyo maana amepewa mkataba,” alisema Dk. Msolla.

“Simba imempa masharti yao ambayo naamini kwa uwezo wake atayatimiza ndani ya mkataba wake, akishindwa wanaweza kufanya maamuzi mengine kwani kila kitu kipo ndani ya uwezo wa kocha huyo, ukiangalia kutetea ubingwa, michuano ya FA, michuano ya klabu bingwa (Caf) vyote vipo ndani ya mwaka mmoja.”

Kwa upande wa Madadi, aliwapongeza Simba kwa uamuzi walioufanya na kuwa unaendana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao kwa kuajiri kocha mwenye sifa zinazotakiwa kwenye ligi kuu.

“Ana sifa zote za kufundisha ligi kuu na ligi yoyote Afrika. Ni kocha ambaye atawasaidia Simba kutimiza malengo yao, ila ili ifikie malengo hayo itategemea na uwezo wake binafsi wa kufundisha, usajili uliofanywa, mahitaji anayopata, programu na ushirikiano wa benchi la ufundi na viongozi.

“Tuliangalia vitu vingi na kingine kikubwa ni uzoefu wake, nchi alizofundisha alifanya nini, elimu ya ukocha, anavyotazamia kushirikiana uzoefu wake, mazingira yetu ya ligi, tulimwangalia hata tabia zake, tuliona anaweza kuwasaidia maana kati ya wote walioomba yeye ndiye aliyepita.”

Hata hivyo, alisema kuwa muda wa mkataba waliompa kocha huyo ni mfupi, lakini wamewashauri Simba kumwongezea mkataba.

Hata hivyo, Kenny Mwaisabula, amekuwa na mtazamo tofauti kuhusiana na ujio wa Mbelgiji huyo akisema Simba ilipaswa kumwamini Kocha Msaidizi, Masoud Djuma.

Alisema Masoud ni mzoefu na soka la Afrika na tayari amezoeana na wachezaji na ndiye aliyechangia mafanikio ya Simba msimu uliopita.

“CV ya kocha mpya si mbaya, majukumu anayopewa naona ni magumu kwani Simba imefanya usajili kwa asilimia kubwa ambao hajahusika, hivyo huenda akashindwa kufikia malengo wakamfukuza. Lakini, kwa wasifu wake atawasaidia sana.

“Nadhani wangemwanini Djuma, ni kocha mzuri ana kila sifa ya kuifundisha Simba ila kwa sababu hizi klabu zina mazoea hayo ni lazima waajiri mzungu. Djuma namwamini kwa kila jambo katika ukocha wake, anawafahamu wachezaji na amefundisha timu kubwa.”