Kawemba, Yono waingia mtego wa Takukuru

Saturday August 12 2017

By Thobias Sebastian, Charles Abel

Dodoma. Wagombea wa nafasi ya ujumbe Saad Kawemba na Yono Stanley walikutana na mkono wa Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa (Takukuru) na kuhojiwa kwa tuhuma za rushwa katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) uliofanyika mjini Dodoma.

Kawemba anayegombea ujumbe wa kanda namba 13, Mkoa wa Dar es Salaam alihojiwa na maofisa hao wa Takukuru jana Ijumaa usiku baada ya kutokuwa na imani naye ingawa baadaye walimwachia.

Maofisa hao ambao walipekuwa mpaka gari hilo la Kawemba, lakini hawakufanikiwa kukuta kitu chochote ambacho kinaweza kuashiria rushwa ambapo waliamua kumwacha huru.

Kawemba anakuwa mgombea wa pili mpaka sasa kukutwa na hekaheka la kuhojiwa kuwa wanaviashiria vya rushwa baada ya Yono Stanley ambaye mpaka sasa yupo chini ya Takukuru kuhojiwa zaidi.

Yono ni mgombea ujumbe nafasi ya uwakilishi kanda namba nane, mikoa ya Ruvuma na Njombe ameshikiliwa na kuhojiwa na taasisi hiyo akidaiwa kutaka kutoa rushwa kwa wajumbe ili wamchague kinyume na sheria.

Taarifa za kushikiliwa pamoja na kuhojiwa kwake zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, RPC Ramadhan Mambosasa alisema mgombea huyo amekutwa na Sh.500,000.

Mambosasa ameongeza kuwa mgombea huyo amekutwa msalani ndani (chooni) nje ya ukumbi wa uchaguzi na alikuwa amezigawa kwenye bahasha zenye kiasi cha Sh 50,000 kwa kila bahasha.

"Ni kweli mgombea huyo anashikiliwa na kuhojiwa na Takukuru kwa tuhuma za kutaka kutoa rushwa kwa wapiga kura ambazo alikutwa na pesa msalani (Chooni), akikutwa na hatia ya kufanya jambo hilo la nia ya kutoa  rushwa sheria zitachukuliwa," alisama Mambosasa.

Awali katika katika hoteli ya St. Gaspar ulinzi wa hali ya juu uliimarishwa mjini Dodoma unapofanyika uchaguzi mkuu wa shirikisho la soka Tanzania (TFF).

Kundi kubwa la maofisa usalama wa jeshi la Polisi waliovaa sare na wale waliovaa mavazi ya kawaida sambamba na wale wa idara ya usalama wa taifa na Takukuru limetanda katika hoteli hiyo katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani bila kuwepo matukio ya uvunjaji sheria.

Askari hao wamekuwa wakifuatilia nyendo za kila mtu aliyepo ndani ya uzio wa hoteli hiyo jambo lililofanya kuwepo na ukimya wa hali ya juu.

Katika kile kinachoonekana ni hofu ya vitendo vya rushwa, jeshi la Polisi limetoa amri kwa wapambe wa wagombea kutoka nje ya hoteli hiyo huku waandishi wa habari wakielekezwa kukaa mbali ukumbi unaofanyikia uchaguzi huo.

"Taarifa zetu za kiinteljensia zinaonyesha kuwa baadhi ya wagombea wamepanga kutumia nyie waandishi wa habari katika kuwahonga wapiga kura hivyo tunawataka mkae mbali na hili eneo ili iwe rahisi kwetu kudhibiti jambo kama hilo," alisema ofisa usalama wa TFF, Inspekta Hashim Abdallah