Katwila awaita mashabiki fainali FA

Muktasari:

Mtibwa Sugar  imetinga fainali ya FA baada ya kuitandika Stand United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Morogoro. Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila  amewaomba mashabiki na wadau mbalimbali wa soka mkoani Morogoro kuisapoti timu hiyo wakati wa fainali ya Kombe la FA ili kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Mtibwa Sugar  imetinga fainali ya FA baada ya kuitandika Stand United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Katwila alisema wachezaji wake wana morali kubwa na mchezo wa fainali ili kutimiza ndoto ya kutwaa kombe hilo na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Katwila alisema benchi la ufundi, wachezaji na wanachama wana lengo moja tu la kutwaa kombe la FA huku wakiwapigia magoti wadau mbalimbali wa soka na mkoa wa Morogoro kiujumla kujitoa  kwenda kuwashangilia kwenye mchezo wa fainali kati ya Singida United au JKT Tanzania.

“Jambo la kwanza tunawaoma wadau mbalimbali wa soka na mashabiki wetu kuanza kujiandaa na safari ya kwenda kuishangilia kwa ari na mali kwenye mchezo wao wa fainali kati ya Singida United ama JKT Tanzania utaopangwa baadaye ili nasi tuweze kupata morali ya juu hatimaye kurudi na kombe la FA Morogoro.”alisema Katwila.

Aliongeza kwa kusema kuwa Mtibwa Sugar haijatwaa kombe kipindi kirefu hivyo kuingia fainali ya FA kumeifanya kufufua ndoto yao ya kutwaa kombe hilo ili kuiwakilisha nchi michezo ya kimataifa.

“Mtibwa Sugar ilitwaa ubingwa Ligi Kuu bara mwaka 1999 na 2002 chini ya kocha wake, John Simkoko na makombe mengine likiwemo la Tusker sasa yupo kocha mkuu, Zubery Katwila kuweka historia ya Mtibwa Sugar kutwaa kombe la FA na tuna kiu na kombe hili.” alisema Katwila.

Katwila alisema wachezaji wawili, Shabaan Nditi na Dickson Daud ndio waliopata bahati ya kutwaa kombe Mtibwa Sugar la Tusker na kuwaomba wadau wa soka kuwaombea dua njema ili kupata ushindi kwenye mchezo wa fainali.