Kasi ya Man City gumzo kila kona

Muktasari:

Timu hiyo imepania kutwaa mataji mawili makubwa msimu huu Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya

LONDON, ENGLAND

Makocha Arsene Wenger wa Arsenal na Antonio Conte wa Chelsea kwa pamoja wamekiri Manchester City si timu ya sayari hii.

Makocha hao wamepagawa baada ya kuona kikosi hicho kinachonolewa na Pep Guardiola kimeshinda mechi 11 kati ya 12 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, lakini kubwa zaidi ni kufunga mabao 40 huku ikifuzu mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema ikiwa bado na mechi mmoja mkononi.

Baada ya kuichapa Leicester City 2-0 Jumamosi iliyopita, kocha Claude Puel alisema Man City ndiyo timu bora kabisa Ulaya kwa sasa, wakati beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown akisema wanaweza kurudia kile kilichofanywa na Gunners huko nyuma, kucheza msimu mzima bila kufungwa.

Sifa hizo zimemfanya Guardiola kuwa na mzuka na kuwaambia mastaa wake, yeyote atakayefanya uzembe na kuvimba kichwa kisha akashindwa kupafomu vizuri, basi atakula naye sahani moja.

“Hakuna mchezomchezo kwenye timu yangu, yeyote atakayeona amekinai na tunachokifanya kwa sasa, namuua,” alisema Guardiola.