Kaseja, Ndikumana tayari kuibeba KMC Ligi Kuu

WAKATI uongozi wa KMC ukitangaza kumsajili kipa mkongwe Juma Kaseja, aliyekuwa nahodha wa Mbao FC, Yusuf Ndikumana, naye imefahamika amemwaga wino ndani ya timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara.

Mwanaspoti inafahamu mbali ya nyota hao wawili waliopewa mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja, KMC pia imemsajili straika wa Mbeya City, Omary Ramadhan ili kukiimarisha kikosi hicho kitakachokuwa chini ya kocha mpya, Etienne Ndayiragije.

Habari zaidi zinasema kuwa baada ya kukamilisha usajili wa nyota hao watatu, viongozi wapo pia kwenye mazungumzo na Hassan Dilunga wa Mtibwa Sugar, Elias Maguli aliye huru na Hassan Kipalatu aliyekuwa Njombe Mji iliyoshuka daraja.

“Ndikumana na Ramadhani wao walisajili wiki iliyopita ila hawajatangazwa bado, huenda viongozi wana sababu zao ila watawatangaza muda wao ukifika, wamesaini mkataba wa mwaka mmoja kila mchezaji, na bado usajili unaendelea kwa ajili ya kuimarisha kikosi maana ligi ina ushindani mkubwa,” kilisema chanzo chetu.

Meneja wa KMC, Walter Urio, alikiri kuna wachezaji wengine watasainishwa na kutangazwa rasmi ila hajawekwa wazi watasajili wangapi kwa ajili ya msimu ujao.

“Inawezekana hao wapo maana usajili unaendelea, kuna nyota wa ndani na wa nje ila tunasubiri mwalimu atakachopendekeza ndicho kinachofanyiwa kazi, ratiba nzima ipo chini ya kocha Ettien kuhusu kuanza kwa kambi yetu,” alisema Walter.