Karia kamishna fainali za CHAN

Muktasari:

Bosi huyo wa TFF aliyechaguliwa Agosti mwaka jana kuchukua mikoba ya Jamal Malinzi ambaye alishindwa kutetea kiti hicho kutokana na kuwa chini ya ulinzi akishikiliwa na makosa mbalimbali.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameteuliwa na Shirikisho la Mpira Barani Africa (CAF) kuwa kamishna wa mechi ya kwanza ya ufunguzi wa fainali za Africa kwa wachezaji wa ndani CHAN.

Karia atasimamia mchezo huo ambao utazikutanisha timu za Morocco na Mauritania utakaochezwa Januari 13 mwaka huu.

Bosi huyo wa TFF aliyechaguliwa Agosti mwaka jana akichukua mikoba ya Jamal Malinzi ambaye alishindwa kutetea kiti hicho kutokana na kuwa chini ya ulinzi akishikiliwa na makosa mbalimbali.

Atausimamia mchezo huo ambao utachezwa kwenye uwanja wa nyasi asilia wa Mohamed V uliopo Casablanca nchini Morocco.

Waamuzi watakaochezesha mchezo huo ni Janny Sikazwe kutoka Zambia atakuwa kati akisaidiwa na msaidizi namba moja kutoka Kenya Marwa Aden Range na msaidizi namba mbili kutoka Msumbiji Arsenio Chandreque Maringula wakati muamuzi wa mezani ni Louis Hakizimana wa Rwanda.

Mchezo huo unaohusisha timu mwenyeji unatarajiwa kufuatiliwa na mashabiki wengi zaidi ambao nbi wenyeji wa Morocco.

Hivi karibuni, Karia aliteuliwa na CAF kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo ya CHAN itakayoanza kutimua vumbi Januari 13 mpaka Februari 4, 2018.

Mashindano hayo, yanafanyika kwa mara ya tano,  bingwa mtetezi ni DR Congo.