Karia hajaulizwa swali lolote

Muktasari:

Nafasi ya Urais Wallace pekee ndiye hakuulizwa maswali baada ya kumaliza kujinadi huku nafasi ya Makamu wa Rais yenye wagombea wanne hakuna pia aliyeulizwa swali.


Dodoma. Wagombea katika uchaguzi wa Shirikisho la soka nchini (TFF) nafasi za Rais na Makamu wa Rais wengi wao hawajakumbana na changamoto ya kuulizwa maswali na wapiga kura baada ya kujinadi na kuomba kura.

Nafasi ya Urais Wallace pekee ndiye hakuulizwa maswali baada ya kumaliza kujinadi huku nafasi ya Makamu wa Rais yenye wagombea wanne hakuna pia aliyeulizwa swali.

Nafasi ya Makamu wa Rais inawagombea Mulamu Ngh'ambi, Michael Wambura, Mtemi Ramadhan na Robert Selasela walijieleza na kuondoka.

Nafasi ya Rais walioulizwa maswali ni mgombea Iman Madega ambaye aliulizwa swali linalohusiana na uhusiano wake na Yanga, Fredrick Mwakalebela, Ally Mayay, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.

Mwakalebela aliulizwa maswali matatu ambayo yote aliyajibu kiufàsaha ambayo ni matumizi ya pesa za FIFA, timu za Taifa na maendeleo ya soka nchini.

Mayay naye aliulizwa maswali matatu ambayo aliyajibu lakini Shija alijikuta yupo katika wakati mgumu alipoulizwa maswali mawili likiwemo swali na kutaja majukumu matano ya Rais pamoja uzoefu wake katika soka.

Shija alijibu kwamba kazi ya Rais ni Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ambapo wajumbe walianza kupiga kelele kuashiria kwamba hawajaridhika na majibu yake huku swali la pili kuhusiana na timu za taifa ambapo alijibu ana uzoefu kwani amecheza mpira na ameongoza sehemu mbalimbali majibu ambayo pia wajumbe hawakuonyesha kuridhika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli aliwapa dakika kila wagombea ambapo nafasi ya Urais walikuwa na dakika tano za kujieleza, nafasi ya Makamu wa Rais walipewa dakika tatu huku wajumbe wakiwa na dakika mbili pekee.

Kuuli alisema kuwa mgombea nafasi ya Makamu wa Rais, Stephen Mwakibolwa jana Ijumaa alituma barua ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.