Kambi ya Ngumi Madola usipime

Muktasari:

Kama ulikuwa unaendelea kuamini ule mwonekano wa awali wa mabondia hao upo vilevile, pole yako. Kwa sasa mabondia hao wamebabadilika sio kwa sababu ya tizi tu, bali hata misosi wanayopiga kila siku katika kambi hiyo.

ACHANA na ile kambi ya mazoezi ya Uwanja wa Ndani ya Taifa, walikokuwa wakiishi mabondia wa timu ya Taifa ya ngumi kwa kuungaunga, kwa sasa kambi ya timu hiyo iliyopo Mkuza, Kibaha Pwani sio ya kitoto unaambiwa.

Kama ulikuwa unaendelea kuamini ule mwonekano wa awali wa mabondia hao upo vilevile, pole yako. Kwa sasa mabondia hao wamebabadilika sio kwa sababu ya tizi tu, bali hata misosi wanayopiga kila siku katika kambi hiyo.

Mwonekano wao wa sasa ni tofauti na ule uliowafanya wachambuliwe hata kwa uzito wa ngumi zao, eti usingeweza kumdodosha mtoto wa miaka 10.

Wako tofauti na sasa wanakupelekewa mizani kwa ajili ya kupunguza uzito, kwani wamejengeka kimazoezi, wanapiga tizi la nguvu na wanakwambia hata akiletwa Floyd Mayweather wazichape naye wala sio ishu sana kwa sasa.

KAMBI YA KIJANJA

Kambi ya timu hiyo inayoundwa na mabondia wanne ipo eneo tulivu la Mkuza nje kidogo ya Mji wa Kibaha zaidi ya kilomita 30 kutoka jijini Dar es Salaam.

Hapo ndiko mabondia hao wamepiga kambi kujiandaa na Michezo ya Madola itakayofanyika kati ya Aprili 4-15 nchini Australia.

Kambi imezungukwa na nyumba chache na miti ndio mingi, japo mabondia wanajifua kwenye Uwanja wa Ndani wa Filbert Bayi ambao una eneo la gym ya kisasa yenye vifaa vyote.

HADI KONI ZINATUMIKA

Nje ya uwanja huo kama ni mgeni, ukifika mlangoni cha kwanza utakachokutana nacho kabla hata ujaingia ndani ni pea kadhaa za padi, glovu na vikinga vichwa.

Ukiingia ndani ya uwanja sasa kuna punching bag mbili zimening’inizwa, pia kumefungwa ulingo wa kisasa na juu ya ulingo ule kuna kamba za mazoezi seti mbili, mipira miwili ya tenisi, koni 10, padi pea nne, glovu pea nne na bandeji ambayo kila bondia anayo ya kwake.

“Vifaa vyote hivyo kila kimoja kina umuhimu wake kwenye mazoezi yetu,” anaanza kueleza Kocha Mkuu, Benjamin Oyombi ambaye mwonekano wake tu unatosha kukuthibitishia anastahili kuwa na leseni ya AIBA ya nyota tatu.

Anasema mipira inayotumika kwenye mchezo wa tenisi na koni kazi yake kubwa ni kuwasaidia mabondia katika mazoezi ya miguu hasa namna ya kujipanga na kukaa sawa ukiwa ulingoni.

“Pad na glovu zinajulikana kazi yake ni kutoa mazoezi ya panchi, kamba yenyewe ina mambo mengi pia lakini kubwa ni kuwajenga katika pumzi.”

RATIBA MATATA

Kila siku asubuhi mabondia hao wana ratiba ya kukimbia kutoka Mkuza ilipo kambi mpaka ilipo kambi ya Jeshi Msangani ambayo kwa mwendo wa bodaboda wenyeji wanakwambia ni unatembea kwa dakika 30.

“Hakuna kutega wala kuishia njiani, ratiba ya kukimbia inaanza saa 12:00 asubuhi,” anasema Nahodha Msaidizi, Haruna Swanga.

Wakati mabondia wakiwa barabarani kwenye mbio, kocha huwa hakai naye anapiga tizi kivyake na mara nyingi anapenda kupiga begi, zoezi analolifanya kwa nusu saa bila kupumzika akiwa na Kocha Msaidizi, David Yombayomba.

“Wanaporejea tunaingia gym ambako wanajifua kwa saa moja kuanzia saa 3:00 kisha wanajiandaa kwa chai au supu asubuhi,” anasema Yombayomba.

Anasema saa 5:00 wanaingia awamu ya pili ya mazoezi yanayofanyika kwa saa tatu mfululizo.

“Kila bondia lazima aruke kamba, apige padi na begi, sparing (mazoezi ya kupigana ana kwa ana) wanafanya lakini sio mara kwa mara kutokana na muda uliosalia kabla hawajaenda kwenye Madola.

Kwenye mazoezi hayo, makocha wote wanapanda juu ya ulingo sanjari na mabondia wawili ambao wanawafanyisha mazoezi ya padi na sparing.

Wengine wawili wanaosalia mmoja anafanya zoezi la kupiga begi na mwingine anaruka kamba, wanafanya hivyo kwa kubadilishana kila baada ya dakika moja.

“Ninachotaka ni kila bondia apitie mkononi kwangu katika zoezi la kupiga padi au sparing,” anasema Oyombi.

Awamu ya pili ya mazoezi inakwisha saa 8:00 na mabondia wanakwenda kuoga na kupata chakula cha mchana kisha wanapumzika hadi saa 10:30 jioni ambako wanarejea kwenye awamu ya tatu ya mazoezi mpaka saa 1:00.

MUDA WA MSOSI SASA

Unakumbuka ule msoto wa kushindia chai na chapati mbili waliopitia mabondia wa timu hiyo? Mambo hayo sasa yamebaki stori tu kwenye kambi hiyo.

“Tunakula chakula tunachotaka sisi, wapishi hutuuliza mnajisikia kula chakula gani kila siku na tunachotamka ndicho tunapikiwa,” anasema Oyombi.

Msosi wao asubuhi kama siosupu ya samaki au kuku basi ni chai ya maziwa, tambi, viazi vitamu, mayai, chapati na matunda au juisi.

Mchana wanakula ugali, wali, samaki, nyama ya ng’ombe, mboga za majani na matunda na usiku ratiba inabadilika wanaweza kula ndizi, tambi, mboga mboga na kuku au samaki na maji ya kutosha.

“Wanapata chakula cha kutosha, wanashiba na muda wa kupumzika pia wa kutosha, katika hilo sina presha,” anasema Oyombi.

Anasema uwezo wa kula msosi zaidi ya sahani moja mabondia hawana, lakini hiyo moja moja wanayokula inakuwa imesheheni.

“Wako katika kipindi cha ‘kukata uzito’ hivyo hawali chakula kingi mno, mwanzo walikuwa wanakula sana lakini sasa wanakula chakula cha wastani,” anasema.

Anafafanua kupunguza uzani kwa mabondia wake ni jambo ambalo linatoa taswira nzuri tofauti na kama ingetokea wangetakiwa kuongeza uzito.

“Unajua unapokata ‘uzito’ unakuwa mwepesi kuliko bondia anayepandisha uzito ambaye kwa vyovyote vile atakuwa mzito ulingoni, maandalizi wanayoyafanya bila shaka tuna medali yetu moja Australia,” anasema Oyombi.

MSIKIE KIDUNDA

Kila bondia aliyeko kambini hapo, ukimuuliza kuhusu mazoezi cha kwanza atakachokujibu ni;

“Huyu kocha achana naye kabisa, jamaa yuko vizuri.”

Nahodha wa timu hiyo, Suleiman Kidunda anasema ujio wa kocha huo ni fursa kwao kwani tofauti yake na wengine imeonekana.

“Hatukuwahi kufanya mazoezi ya nguvu namna hii, ila tangu kocha huyo amejiunga nasi tunajiona tofauti, mwanzoni tuliona kama mateso lakini sasa tumezoea tunaona kawaida,” anasema Kidunda.

Anasema kwa mazoezi waliyoyafanya, namna walivyobadilika kiwango chao na hamasa wanayopewa na kocha anaamini kwenye michezo ya msimu huu ni nafasi yao kufanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka 1998 ambapo Michael Yombayomba (marehemu) alitwaa medali ya dhahabu ya Madola.