Kama utani Yanga yawachia ubingwa Simba, Azam

Muktasari:

Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara mara 27 tangu 1965

Dar es Salaam. Mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu 2018-19 zimeanza rasmi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa ratiba.

Pamoja na ratiba hiyo kutoka mbio za ubingwa msimu ujao zinaweza kuwa za timu mbili Simba na Azam kutokana na usajili maandalizi yao kulinganisha na mabingwa wa kihistoria Yanga.

Tangu kufunguliwa dirisha la usajili msimu huu, Simba, Azam zimekuwa bize katika kutegeneza vikosi vyao wakati Yanga ipo kimya kabisa.

Ukiangalia maandalizi ya timu zote msimu huu ambao utakuwa na timu 20, ni wazi Ligi Kuu Bara itakuwa na ushindani mkubwa kupata timu itakayocheza Ligi ya Mabingwa pamoja na Kombe la FA anapotoka mwakilishi mwingine Kombe la Shirikisho Afrika.

Kuongezeka kwa idadi ya timu ni wazi klabu inayotaka tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani ni lazima kuwa na kikosi kipana na benchi bora la ufundi.

SIMBA

Mabingwa watetezi wameonja asali wanataka kuchonga mzinga kwa kuhakikisha wanachukua  tena  ubingwa huo msimu huu.

Katika kukamilisha hilo Simba imemwajiri kocha Mbelgiji, Patrick Aussems mwenye rekodi ya kuvutia barani Afrika pia imesajili wachezaji wapya 9 hadi sasa.

 Msimu uliopita washambuliaji wao wawili Emmanuel Okwi na John Bocco walifunga mabao 34 katika Ligi Kuu, lakini msimu huu wameongeza washambuliaji wengine  watano.

Washambuliaji wapya waliosajiliwa Simba, Meddie Kagere, Adam Salamba, Mohamed Rashid, Marcel Kaheza  na Abdul Suleiman wote wameonyesha uwezo mkubwa wa kuzifumani nyavu katika mashindano ya Kombe la Kagame.

Safu ya kiungo imeimalishwa kwa kuongeza Mzambia  Clatous Chama huku Hassan Dilunga akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wake.

Pamoja na kuwa na beki bora msimu uliopita, Simba imemsajili mkongwe Pascal Wawa katika safu ya ulinzi huku wakimrudisha kundini kipa wao wa zamani Deo Munishi 'Dida' aliyekuwa akicheza soka la kulipwa Afrika Kusini.

AZAM

Matajiri wa Chamazi walichokifanya katika Kombe la Kagame ni wazi wametuma salamu kwamba msimu huu wamepania kufanya kitu katika Ligi Kuu.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu 2012-13, Azam wamejimalisha kuwa kumchukua kocha wa zamani wa Singida United na Yanga Mdachi Hans Pluijm.

Pluijm mwenye rekodi nzuri katika soka la Tanzania baada ya kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili na Kombe la FA moja pamoja kuwavusha kwa mara ya kwanza Yanga kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Mdachi huyo ameimalisha benchi lake kwa kumchukua kocha Juma Mwambusi pamoja na Idd Cheche kuhakikisha wanategeneza rekodi mpya Chamazi.

Mdachi huyo amewasajili watu wa kazi nyota aliofanya nao kazi kwa mafanikio kiungo Mudathir Yahya, mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma pamoja na kiungo Tafadzwa Kutinyu.

Katika ngome yake amefanikiwa kupata saini ya Hassan Mwasapili kutoka Mbeya City,  Mganda Nicco Wadada pamoja na mshambuliaji Ditram Nchimbi.

YANGA

Yanga inayoshiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho inasumbuliwa na tatizo la fedha jambo linalofanya kushindwa kujianda vizuri kulinganisha na wapinzani wao katika mbio za ubingwa.

Mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, Yanga haina kocha mkuu kwani Mkongo Mwinyi Zahera bado hana vibari vya kufanya kazi.

Yanga inayosifika kwa kusajili nyota mbalimbali msimu hadi sasa imesajili wachezaji watatu kati yao wawili ni nyota wao wa zamani.

Yanga imefanikiwa kumsajili Mrisho Ngassa kutoka Ndanda pamoja na Deus Kaseke akitokea Singida United baada ya kumaliza mkataba wake.

Mchezaji mpya aliyesajili na Yanga ni kiungo Feisal Salum kutoka JKU ya Zanzibar.

Pamoja na matatizo yote ya Yanga uwezi kuwaondoa katika mbio za ubingwa kutokana na historia yao kuwa na kikosi kilichokaa pamoja kwa muda mrefu.

Kubwa zaidi iwapo watamaliza matatizo yao ya fedha za mishahara ya wachezaji wao basi lolote linaweza kutokena.

SINGIDA UNITED

Kikosi cha Hemed Morocco kinakazi kubwa kufikia mafanikio yake ya msimu uliopita waliomaliza nafasi ya tano katika Ligi Kuu pamoja na kucheza fainali ya Kombe la FA.

Singida United imepoteza nyota wake wengi kwa sababu mbalimbali pia wamepoteza nguvu zao fedha walizoanza nazo msimu uliopita.

Pamoja na kuonekana kuwa bize kusajili tangu lilipofunguliwa dirisha la usajili ni wachezaji wanne waliongezwa kikosini.

Wachezaji hao ni kipa David Kisu, washambuliaji Habib Kyombo, Tiba John na beki Boniphace Maganga huku wale wachezaji wa kimataifa iliyowasajili imwafungulia milango ya kuondoka.

MTIBWA SUGAR

Mabingwa wa Kombe la FA, baada ya kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho mwaka huu wenyewe wamemsajili mchezaji mmoja.

Mtibwa Sugar wamemrudisha kundini mshambuliaji wao Juma Luizio akitokea Simba, huku wakibaki na kikosi chao kilekile.

Hata hivyo Mtibwa tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu 2000 imekuwa ni timu inayosindikiza wenzake katika ligi kwa mara zote imekuwa ni miongoni mwa timu sita bora.

Udogo wa kikosi hicho cha Zuberi Katwila na kushiriki mashindano mengi Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Shirishisho Afrika kwa wakati mmoja ni wazi hawana nafasi ya kushindani ubingwa.