Kama utani Yanga inamkosa straika

Muktasari:

Lakini hilo litaendelea kuwa ndoto kwani mipango hiyo imekufa rasmi baada ya straika huyo kuamua kubaki kikosini mwake baada ya kuumwa sikio ajifunze kwa kile kilichomkuta aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya, aliyezimika tangu atue Yanga.

HUENDA mashabiki wa Yanga wasiifurahie habari hii, lakini ndivyo ilivyo. Mashabiki hao wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara walikuwa wakijiandaa kumpokea mfumania nyavu mahiri wa Prisons, Mohammed Rashid.

Lakini hilo litaendelea kuwa ndoto kwani mipango hiyo imekufa rasmi baada ya straika huyo kuamua kubaki kikosini mwake baada ya kuumwa sikio ajifunze kwa kile kilichomkuta aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya, aliyezimika tangu atue Yanga.

Ipo hivi. Straika huyo ameanza mazoezi na timu yake kutokana na kujazwa upepo na watu wake wa karibu kwa kumwambia amuangalie Kakolanya anavyosota benchi Jangwani, huku akizungushwa kulipwa fedha zake za usajili hadi sasa.

Habari za ndani zilizovujishwa na mtu wa karibu wa straika huyo mwenye mabao sita hadi sasa msimu huu akilingana na Obrey Chirwa, ni kwamba Rashid ameambiwa kama anataka kuua kipaji chake basi aende Yanga na akisisitizwa kuwa, hata fedha anazoahidiwa sasa na mabosi wa Jangwani huenda asizipate kama Kakolanya.

Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed ‘Bares’ alisema hakuwa na taarifa za straika huyo kuondoka kikosini, ndio maana hashangai kumuona mazoezini na wenzake.

“Sina taarifa za kuondoka kwake (Rashid) ila ninachoweza kukujulisha yupo mazoezini na wenzake tangu jana (juzi) na ataendelea kubaki Prisons hadi mwisho wa msimu,” alisema Kocha Bares aliyemsajili mkali huyo wa mabao.

Domayo kuna kitu

Wakati hayo yakiendelea zipo taarifa kuwa kiungo wa zamani wa Yanga, Frank Domayo ‘Chumvi’ anajiandaa kurudi Jangwani kutoka Azam FC.

Mtu wa karibu wa mchezaji huyo amesema: “Yanga imekuwa ikimfuatilia kwa ukaribu Domayo wakimtaka arudi kikosini kwao, lakini mwenyewe bado hajafanya maamuzi.”

Jamaa huyo aliongeza na kusema, Domayo anashindwa kufanya maamuzi kwa sababu akili yake bado anaifikiria Azam iliyompokea akiwa majeruhi na kumtibia mpaka akapona, japo mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu.

Domayo alipoulizwa na Mwanaspoti alijibu kwa kifupi; “Mimi ni mchezaji wa Azam na habari za Yanga hata sizijui, kama zipo mtajua tu niacheni nifanye kazi kwanza.”

Domayo mwenye miaka 24, aliibuliwa na JKT Ruvu mwaka 2012 kabla ya kutua Yanga aliyoichezea miaka miwili hadi 2014, baada ya hapo alisajiliwa na Azam.