Kakolanya yupo vizuri

KIPA wa Yanga, Beno Kakolanya, hajacheza mechi yoyote tangu Ligi Kuu  Bara msimu huu ianze kwa vile ni majeruhi, lakini ametaja mambo matatu yaliyobadilika katika maisha yake mara baada ya kutua Yanga.

Kakolanya aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Prisons, amesema kwa sasa yupo vizuri mno kiuchumi, ubora wa kazi na kujulikana tofauti na alivyokuwa kwa maafande hao wa Magereza.

“Kipato ninachokipata Yanga ni tofauti na nilichokuwa nacho Prisons, hii ni hatua moja mbele, kazi zangu ni bora kulingana na aina ya timu inayosaka ubingwa kila mwaka na inanifanya nionekane bora zaidi,” alisema.

“Hata nikiwa mitaani mashabiki wananiongezea mzuka, inadhihirisha namna gani ninavyofuatiliwa.”

Kuhusu hali yake,  alisema anaendelea vyema baada ya kuwa nje ya uwanja baada ya kuumia goti akiwa na Taifa Stars iliposhiriki Kombe la Cosafa.