Kagere freshi, Salamba ajipange

Muktasari:

Mohammed Banka, amesema Kagere ameonyesha uwezo wa hali ya juu kwa muda mfupi kiasi hata watakapokosekana akina John Bocco na Emmanuel Okwi, pengo halitaonekana na kuwataka wachezaji wengine wapya waliosajiliwa wajipange.

WAKATI mashabiki wa Simba wakisubiri kwa hamu kuuona mziki mnene wa kikosi chao katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, aliyekuwa kiungo wa timu hiyo amefichua ni Meddie Kagere tu aliyeonyesha anastahili kukipiga Msimbazi.

Mohammed Banka, amesema Kagere ameonyesha uwezo wa hali ya juu kwa muda mfupi kiasi hata watakapokosekana akina John Bocco na Emmanuel Okwi, pengo halitaonekana na kuwataka wachezaji wengine wapya waliosajiliwa wajipange.

Banka alisema jinsi Kagere alivyopambana katika michuano ya Kombe la Kagame, inaonyesha ni mchezaji mwenye kuheshimu hadhi yake hali itakayomfanya bidii yake iwe kubwa kwa ligi ijayo, hicho ndicho anachokifanya Okwi kulinda heshima yake.

“Kagere naona atakuwa msaada mkubwa hata atakapokosekana Okwi, anajua kupambana na kuzitumia kikamilifu dakika 90 anapokuwa dimbani, hii inaonyesha anajua anachokifanya,” alisema Banka.

“Akikutana wachezaji wazoefu ambao wapo kwenye kiwango cha juu kama Jonas Mkude au Shiza Kichuya ambao watakuwa wanapandisha mashambulizi, Kagere atakuwa na hatua nyingine zaidi ya alivyofanya Kagame.”

Juu ya nyota wengine akiwamo Adam Salamba, Marcel Kaheza na Mohammed Rashid, Banka alisema wanatakiwa wajipange na kujifunza kile alichokifanya Kagere ili wajihakikishie namba ndani ya kikosi cha kwanza.

“Bila shaka hao kina Mo Rashid, Salamba na Kaheza watakuwa wamejua wanapaswa wafanye nini, kwani kocha aliwapa nafasi lakini bado hawajaonyesha kitu ndio maana nasema wajipange kweli kweli kabla msimu haujaanza,” aliongeza.

Hata hivyo, Mo Rashid alisema hana hofu kuhusiana na ushindani wa namba kwa madai anaamini atakuwa na nafasi ya kucheza mbele ya Bocco, Okwi na Kagere, akisisitiza mchawi ni mazoezi.

“Kwani wao wamewezaje kuwa walivyo leo, halafu mimi nishindwe kufikia mafanikio hayo, asikwambie mtu mchawi ni mazoezi na kuzingatia miiko ya soka, hivyo ndivyo vitamfanya mtu afike mbali,” alisema straika huyo toka Prisons.