Kagere, Bocco wampa mzuka Mbelgiji

Muktasari:

  • Katika mazoezi hayo nyota watatu wa Kimataifa Cletus Chama (Zambia), Meddie Kagere (Rwanda) na Emmanuel Okwi (Uganda) watakosekana kutokana wakitokea katika majukumu ya timu zao za Taifa.

Dar es Salaam. Simba inaendelea na mazoezi uwanja wa Boko Veterans kujiandaa na mechi ya Jumamosi Septemba 15, dhidi ya Ndanda mjini Mtwara.

Katika mazoezi hayo nyota watatu wa Kimataifa Cletus Chama (Zambia), Meddie Kagere (Rwanda) na Emmanuel Okwi (Uganda) watakosekana kutokana wakitokea katika majukumu ya timu zao za Taifa.

Nyota hao watarudi nchini kesho Jumatano Septemba 12 kila mmoja kwa muda wake na watakwenda moja kwa moja kambini katika hoteli ya Sea Scape ambapo Alhamisi watakuwa miongoni mwa msafara utakaoondoka saa 1:00 asubuhi kuelekwea Mtwara.

Kagere anarudi nchini akitoka Rwanda ambako alicheza mechi ya kufuzu kombe la Mataifa Afrika Afcon dhidi ya Ivory Coast na kupoteza kwa bao 2-1.

Rwanda walipata bao hilo kupitia kwa Kagere ambaye anafunga katika mechi ya tano mfululizo za kimashindano ukianzia ngazi ya klabu yake Simba ambayo walimsajili akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Kagere amefunga mechi ya fainali dhidi ya Azam bao moja wakipoteza kwa bao 2-1, Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 na mechi mbili za Ligi ambazo wamecheza dhidi ya Tanzania Prison na Mbeya City.

Wakati Kagere akiendeleza moto wake wa kufunga, Simba walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya AFC Leopards Jumamosi na kuwafunga mabao 4-2 yakifungwa na John Bocco mawili ambaye alifungua akaunti ya mabao na Mohammed Ibrahim 'MO' ambaye ndio amerudi katika ubora wake na Marcel Kaheza.

Bocco ambaye hakufunga bao lolote katika mechi mbili za Ligi ambazo Simba wamecheza mara baada ya kufunga katika mechi ya kirafiki yamempa mzuka kocha wa Simba Mbeligiji Patrick Aussems na kuamini kwamba eneo la ushambuliaji linazidi kuimarika.

Mbeligiji Aussems alisema kocha yoyote anatamani kuwa na washambuliaji kama Kagere, Bocco na Okwi kwani wana uwezo na wanaweza kufunga na kubadili matokeo muda wowote katika aina yoyote ya mechi.

Anasema: "Tumecheza mechi mbili za Ligi tumefunga mabao matatu ambayo yote yamefungwa na Kagere ambaye nina imani kubwa ataendeleza kasi ya kufunga katika mechi nyingi, lakini Bocco baada ya kufunga mabao mawili mechi ya kirafiki atakuwa hana presha tofauti na alivyokuwa hajafunga na atacheza kwa utulivu.

"Kufunga kwa Kagere na Bocco katika mechi za mwisho walizocheza naona wakikutana pamoja wataendeleza hilo, lakini hata Okwi hakufunga mechi ya Uganda lakini alicheza vizuri tofauti na nilivyotogemea kwani alitoka majeruhi," alisema.

"Tangu nimefika hapa hawajacheza pamoja katika mechi yoyote ya kimashindano na kama wakiwa fiti wote mechi moja naona kuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri kati yao," alisema Aussems.