Kagere, Bocco, Okwi wapotezwa Nangwanda

Muktasari:

Kabla ya mechi ya leo Simba imeifunga Ndanda katika mechi nane mfululizo za Ligi Kuu

Mtwara. Pamoja na Simba kuanza na washambuliaji watatu Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi wameshindwa kuzigusa nyavu za Ndanda Fc wakilazimishwa suluhu kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mtwara.

Matokeo hayo yanaifanya Ndanda FC kufuta uteja wake wa kufungwa mechi tisa ilichoza dhidi ya Simba tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo huo Simba ilitawala mchezo lakini washambuliaji wake hao watatu walishindwa kuipenya ngome ya Ndanda.

Ndanda tangu walivyopanda kucheza ligi kuu msimu 2014-15 hawajawahi kupata hata sare kwa maana hiyo matokeo haya watakuwa wamevunja mwiko.

Simba mbali ya kutawala katika kipindi cha kwanza kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, lakini walishindwa kufunga hata bao la kuotea.

Mabeki wa kati wa Ndanda, Malika Ndeule na Rajabu Rashid waliweza kuwaweka chini ya ulinzi watatu hao.

Huenda Bocco, Kagere na Okwi kucheza wote kwa mara ya kwanza katika mechi moja.

Simba walianza kutengeneza nafasi ya kufunga dakika ya nne baada ya kupigwa shuti na Tshabalala nje ya boksi ambalo likapaa, Simba waliendelea na dakika ya 15 krosi ya Kapombe Okwi alipiga kichwa lakini kilitoka nje.

Dakika ya 16 MO Ibrahim alipiga krosi nyingine ambayo iliunganishwa kwa kichwa na Kagere kilitoka nje.

Simba waliendelea na mashambulizi kwa kutumia mipira ya krosi na dakika ya 19 Kagere alipiga kichwa krosi ya Okwi lakini kilitoka nje, dakika 35 Bocco aliunganisha krosi ya Kichuya ambayo ilizaa piga nikupige lakini shuti lake lilotoka.

Dakika ya 39 Simba walipata faulo iliyokwenda kuchungwa na Tshabalala ambayo iliunganishwa na kichwa cha Wawa ambacho kilikwenda kumkuta Bocco ambaye kama angekuwa makini angeweza kuiandikia Simba bao la kuongoza.

Ndanda wao hawakuwa na mashambulizi ya mara kwa mara kwani walikwenda golini kwa Simba kwa kushtukiza.

Muda mwingi kipa wa Simba Manula alikuwa katika wakati salama kwani mashambulizi kwake yalikuwa yabkawaida na alikuwa akidaka mipira ambayo haikuwa hatarishi.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika mbali ya Simba kushambulia mara kwa mara na Ndanda kufanya hivyo kwa kushtukiza lakini kilimalizika bila bao.