Kagera Sugar mambo magumu, Kavila awatuliza

Muktasari:

  • Msimu uliopita Kagera ilicheza mechi tisa za kwanza za Ligi Kuu bila kushinda

 Mwanza. Kagera Sugar inaendelea kujiandaa jijini Mwanza kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu, lakini katika mechi zake za kirafiki ilizocheza haijaonja ushindi wowote, jambo lilomuibua nahodha wake George Kavila kuwatoa hofu mashabiki wao.

Timu hiyo katika msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kuanza vibaya Ligi na baadaye kuamka dakika za mwisho na kusalimika.

Tayari ‘Wanankurukumbi’ hao wameshajitupa uwanjani mara tatu na kupoteza mechi mbili na sare moja, ambapo awali walilala 2-1 dhidi ya Alliance FC,wakatoka sare ya 1-1 na Singida United kisha kulazwa 2-0 na Mbao.

Nahodha Kavila amewatoa hofu mashabiki wao kuwa wasikate tamaa na badala yake wasubiri ligi ianze waone muziki wao na watafurahi.

Alisema kuwa timu hiyo inakuja kwa kasi msimu ujao na matokeo hayo waliyoyapata kwenye mechi zao za kirafiki haziwaumizi kichwa au kuwakatisha tamaa.

“Hizi ni mechi tu za kirafiki wala haziwezi kutukatisha tamaa, mashabiki watulie wasubiri ligi ianze tumejipanga kuja kwa kasi kuhakikisha tunafanya vizuri kila mechi,” alisema Kavila.

Mkongwe huyo aliongeza kuwa kwa tathimini yake na timu walizokutana nazo kwenye mechi za kujipima nguvu, amebaini klabu kujipanga vyema na kwamba ushindani utakuwa mkali.

“Timu zimejipanga vizuri na zinaonyesha hali ya ushindani hapo baadaye kwahiyo na sisi tutajipanga kuja kiushindani zaidi,”alisema Mkongwe huyo.