Zimamoto yachezea kichapo

Muktasari:

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan Mjini hapa ulishudiwa na idadi ndogo ya mashabiki waliojitokeza kiwanjani hapo.

Zanzibar. Maafande wa KVZ imewaziba mdomo wapenzi na mashabiki wa Zimamoto baada ya kuirarua kwa mabao 4-2 katika mchezo wa Ligi Kuu Zanzibar kanda ya Unguja.
Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Amaan Mjini hapa ulishudiwa na idadi ndogo ya mashabiki waliojitokeza kiwanjani hapo.
Mbali ya mchezo huo kuonekana kukosa mashabaki , lakini timu hizo ambazo zote ni waajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilionekana kucheza mchezo wa upinzani wa hali ya juu hasa katika kipindi cha pili.
Mshambuliaji wa Salum Songoro wa KVZ alikuwa mwiba mchungu kwa Zimamoto baada ya kufunga mabao matatu katika dakika ya 9, 16 na 42 kabla ya Sultan Juma hajakamilisha bao la nne katika dakika ya 61 ya mchezo huo.
Mabao ya kufutia machozi kwa Zimamoto yalifungwa na Othman Denge katika dakika ya 63 na Idrissa Simai (88) na kufanya mchezo huo kumalizika kwa mabao 4-2.
Katika mchezo wa awali uliopigwa kiwanjani hapo kati ya Taifa ya Jang’ombe na Polisi ulimalizika kwa suluhu .
Ligi kuu Zanzibar inaendeleo leo kwa kupigwa michezo miwili ambapo Kipanga watashuka kiwanjani kukipiga na Charawe saa 10.00 jioni, wakati KMKM wakipepetana na Kilimani City michezo yote itapigwa Uwanja wa Amaan Mjini hapa.