KUVUNA Mil 100

Muktasari:

Mabosi hao wameamua kuwatengea nyota hao kiasi cha Sh100 milioni ili kuhakikisha wanaweka rekodi ya kuvunja mwiko wa kukaa muda mrefu bila kubeba taji la Ligi Kuu Bara (VPL).

MABOSI wa Simba wajanja bwana. Jamaa hao wana akili sana na kwa kuwa hawataki kupishana tena na taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, wamewatengea fungu la maana nyota wao Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya ili kuwapa mzuka Bara.

Mabosi hao wameamua kuwatengea nyota hao kiasi cha Sh100 milioni ili kuhakikisha wanaweka rekodi ya kuvunja mwiko wa kukaa muda mrefu bila kubeba taji la Ligi Kuu Bara (VPL).

Simba ina msimu wa tano sasa haijabeba ndoo ya VPL. Mara ya mwisho kubeba taji hilo ilikuwa msimu wa 2011-2012 wakati huo Jonas Mkude akiwa kinda ndani ya kikosi hicho akitokea kupandishwa timu ya Vijana U-20.

Kama mnavyojua, Simba ndio kinara wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na alama 46 sawa na Yanga, ila uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa unaibeba mbali na mechi mbili za mkononi ilizonazo kabla ya kuvaana na watani zao wakati ligi ikiwa raundi ya 22.

Simba itaanza kula viporo vyake Aprili 3 kwa kuvaana na Njombe Mji kabla ya kusubiri kuvaana na Mtibwa Sugar ambao pia ni kiporo cha Yanga.

Kutokana na kasi kubwa ya watani zao Yanga, Simba imeamua kufanya mambo yake kwa ustadi mkubwa ikiwamo kuweka mezani fungu hilo la fedha.

ISHU IPO HIVI

Kwa utaratibu wa Simba, katika kila mechi inayoshinda wachezaji hupewa Sh10 milioni kama posho ili wagawane na sasa uongozi wa timu hiyo umesisitiza Mil 100 ziko tayari na ni wachezaji tu kuamua kushinda mechi zilizosalia ili kubeba taji Msimbazi na pia kuvuna mkwanja huo.

Fedha hizo hutolewa mara tu baada ya wachezaji kushinda mechi na Meneja wa timu hiyo, Richard Robert ndiye huenda uwanjani na fungu hilo ili kuwamwagia nyota wa Msimbazi.

Kwa hesabu zilivyo ni; kwamba nyota wa Msimbazi wamevuna kiasi cha Sh130 milioni mpaka sasa kwa kushinda mechi 13, hiyo ikiwa ni posho tu, achilia mbali mishahara na marupurupu mengine.

Wachezaji hao wamepoteza posho hizo kwenye mechi saba ambazo wametoka sare dhidi ya Azam, Yanga, Mtibwa Sugar, Stand United, Mwadui, Lipuli na Mbao FC .

Hata hivyo kwa sasa wamepania kuweka fungu hilo mfukoni kwa kupeleka furaha ya ubingwa Msimbazi.

MSIKIE MANARA

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amesisitiza posho za wachezaji hao zipo na wanachopaswa kufanya ni kupambana tu ili waweze kushinda mechi zilizosalia.

“Tumekuwa tukitoa posho hizo za Sh10 milioni tangu msimu umeanza. Ni utaratibu wa kawaida kwenye timu yetu na wachezaji wote wanafahamu kuwa wakishinda mchezo mmoja wanaweza kupata kiasi gani cha fedha,” alisema.

Hata hivyo, wanaweza kuvuna zaidi kwenye mechi dhidi ya Yanga kutokana na uzito wa mchezo wenyewe. Mara nyingi kwenye mechi ya watani huwekewa kati ya Sh20 hadi 40 milioni ili kuwaongezea morali. Simba inahitaji kushinda dhidi ya Yanga ili kuongeza wigo wa pointi baina yao na kujiweka kwenye njia nzuri ya kutwaa taji.

YAPANIA VIPORO

Simba tayari imepangiwa ratiba ya viporo, itacheza ugenini dhidi ya Njombe Mji Aprili 3 na kisha kukipiga na Mtibwa siku tano baadaye mjini Morogoro.

Manara alisema kwa sasa wamejidhatiti kupata pointi hizo sita ugenini kwa kushinda mechi zote mbili na mipango yao ya ndani na nje ya uwanja iko vizuri.