KMC yawatibulia Msimbazi

MABOSI wa Simba waliokuwa wakifanya maandalizi ya kuipokea timu yao iliyotarajiwa kuwasili alfajiri ya leo kutoka Uturuki, wamejikuta wakipata ganzi baada ya timu iliyopanda Ligi Kuu, KMC kuiwatibulia kwenye kambi yao.

Simba imezoea kuweka kambi hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam hivyo jana Jumapili mabosi wake walienda huko ili kuweka mambo sawa wakati wakiisubiri timu, lakini walikutana na taarifa kwamba KMC wamejaa tele hotelini hapo.

Inaelezwa kuwa kitendo cha KMC kujichimbia hotelini hapo kiliwafanya mabosi hao kupagawa na kulazimika kuangalia ustaarabu mwingine wa kuiweka timu yao kambini na fasta wakakimbilia Serena Hotel ili kutuliza kwanza akili.

Mwanaspoti imedokezwa kuwa mmoja wa kiongozi wa juu wa Simba baada ya kupata taarifa hizo, aliamua kutafuta utatuzi wa haraka ili kutafuta chimbo jingine kwa vile hawapendi kukaa kambi moja na timu nyingine.

Inaelezwa imeamuliwa kuwa watarudi Kunduchi mara baada ya mchezo wao wa kimataifa wa Simba Day dhidi ya Asante Kotoko na iwapo tu KMC watakuwa wameshatimka hapo, vinginevyo wataangalia ustaarabu mwingine.

“Kwenda pale ni baada ya mechi ya Kotoko, kwa sasa hapana, ila tumepanga kuongea na wenye hoteli ile ili kuwekana sawa kwani tunahofia isije tukawa kwenye mechi za kimataifa ikatokea jambo kama hili,” chanzo chetu toka ndani ya Simba kilidokeza.

Kuhusu msafara wa timu, Meneja wa Simba, Richard Robert, alisema Kocha Mkuu, Patrick Aussems, alitarajiwa kuongoza kikosi cha wachezaji kuingia nchini usiku wa kuamkia leo Jumatatu baada ya jana kuondoka Uturuki majira ya saa 4 asubuhi.

“Msafara wa kwanza utaenda Serena Hotel kuweka kambi mpaka tutakapocheza na Asante Kotoko, kisha tutawapa wachezaji mapumziko mafupi na tutarudi kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Ngao ya hisani,” alisema Robert.

Meneja huyo aliongeza msafara wa pili na mwisho wa Simba utaingia mchana wa leo ukiwa ni watu wa benchi la Ufundi waliowahi kuondoka Uturuki jana, ila ndege yao ikiwa na mizinguko mirefu tofauti na ile ya Shirika la Ndege la Uturuki iliyobeba wachezaji.

Msafara wa mchana utakaotumia Emirates utakuwa naye (Meneja), Kocha Msaidizi Masoud Djuma, Daktari Yassin Gembe, Mtunza Vifaa, Hamis Mtambo na Kocha wa Makipa Muharami Mohammed ‘Shilton’.

Naye Kocha Masoud Djuma alifichua kwa sasa habari ya kikosi chao ni kazi ya Kocha Mkuu.

“Sina mengi ya kuzungumza kwani mwenye jukumu la kuzungumzia masuala ya ufundi ni la Kocha Mkuu, ila tunaamini maandalizi tuliyofanya Uturuki yatasaidia kuifanya timu iwe tishio kwa msimu ujao, ngoja turudi,” alisema Kocha Djuma.

“Kambi ilikuwa nzuri na vijana walipata muda wa kutosha wa kujiandaa, naamini ligi itakapoanza kila mmoja ataiona timu yetu ilivyo.

MECHI IJAYO:

Kirafiki Simba Day...

Keshokutwa J’tano,

Simba vs Asante Kotoko.

Saa 10:00 jioni...Taifa