KMC yawatega mastaa

Muktasari:

  • Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison aliliambia Mwanaspoti kuwa lengo la kuwasajili nyota wapya kwa mkataba wa miezi 12 kila mmoja, unalenga kuleta ushindani na ufanisi kwenye kikosi chao pamoja na kukwepa gharama zisizo na ulazima.

WAKATI idadi kubwa ya klabu ikisajili wachezaji kwa mikataba yenye urefu wa miaka miwili, uongozi wa KMC umefichua sababu zilizopelekea iwasajili baadhi ya mastaa wanaotamba nchini kwa mkataba mfupi wa mwaka mmoja.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison aliliambia Mwanaspoti kuwa lengo la kuwasajili nyota wapya kwa mkataba wa miezi 12 kila mmoja, unalenga kuleta ushindani na ufanisi kwenye kikosi chao pamoja na kukwepa gharama zisizo na ulazima.
"Wazo la kusajili mchezaji kwa mkataba wa mwaka mmoja limetolewa na Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije ambaye alitupa sababu za msingi za kwa nini tusiwape wachezaji tunaowasajili mikataba mirefu.
Kwanza kocha alipendekeza hilo ili kuwafanya wachezaji wasibweteke. Kama unavyofahamu wachezaji wengi wa Kitanzania wamekuwa wakiridhika pale wanapokuwa na mikataba mirefu wakiamini hata wasipopata nafasi ya kucheza, haiwezi kuvunjwa na kama ikivunjwa watalipwa hela ambazo hawajazitolea jasho.
Kwa kulizingatia hilo, mwalimu anaamini kuwa mchezaji akiwa na mkataba mfupi, atajituma na kupambana ili aongezewe mkataba mpya lakini kingine, uamuzi huu unalenga kuipunguzia timu mzigo wa gharama ambazo itaingia pindi mchezaji akivunjiwa mkataba," alisema Harrison.
Nyota waliosajiliwa na KMC kwa mkataba wa mwaka mmoja ni Juma Kaseja aliyetokea Kagera Sugar, Ally Ally na Aron Lulambo (Stand United), Hamis Abdallah (Sony Sugar) na kiungo Abdulhalim Humud aliyeongezewa mkataba wa kuendelea kuitumikia tiu hiyo.