KIWANGO, Makipa hawa ni moto VPL

Muktasari:

Sasa huyo Popat unaambiwa ana historia ya kipekee. Kwenye klabu yake ya Yanga alianza kucheza akiwa kipa kabla ya kubadili nafasi na kuwa straika matata. Unaambiwa alikuwa kipa wa kiwango cha juu enzi zake.

Dar es Salaam. UNAMFAHAMU Kitwana Manara ‘Popat’? Yawezekana haumfahamu na wala hujawahi kumsikia. Pengine unamfahamu zaidi Sunday Manara ‘Computer’ ambaye ndiye maarufu zaidi.

Sasa huyo Popat unaambiwa ana historia ya kipekee. Kwenye klabu yake ya Yanga alianza kucheza akiwa kipa kabla ya kubadili nafasi na kuwa straika matata. Unaambiwa alikuwa kipa wa kiwango cha juu enzi zake.

Huyu ndiye Popat, ndugu wa Sunday Manara. Ni Baba Mdogo wa huyu Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ambaye huwa anachonga kinoma. Kwao mpira ndio nyumbani, baba zake wameucheza, Haji anauzungumza.

Ukiachana na Popat, Tanzania, imewahi kushuhudia makipa wengine wa maana kama Athumani Mambosasa, Juma Pondamali, Iddi Pazi, Mohamed Mwameja na wengineo. Walitikisa kinoma.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni ni kama makipa wameshuka hivi. Viwango vyao vinatajwa kuwa chini kulinganisha na wale wa awali. Pamoja na yote, Ligi Kuu Bara (VPL) sasa ina makipa wanaofanya vizuri, na makala hii imewaangazia.

Aishi Manula-Simba

Kipa wa Simba, Aishi Manula, si mtu wa mchezo mchezo. Kipa huyo ametua Simba akitokea Azam FC na ameweza kucheza mechi zote za Ligi Kuu pamoja na za mashindano ya kimataifa.

Unaambiwa makipa wengine wa Simba; Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja, wanasubiri siku akiumia ndio wacheze, vinginevyo jamaa si mtu wa kuwekwa benchi kabisa.

Mpaka sasa msimu huu Manula ameshacheza mechi zote 25 za Ligi Kuu na kuruhuusu mabao 13 tu. Na unaambiwa wikiendi hii anatarajiwa kusimama langoni pale Simba itakapovaana na Yanga.

Anachokifanya kipa huyo msimu huu ni mwendelezo wa alichofanya misimu miwili iliyopita ambapo alitwaa tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu.

Msimu huu hakuna ubishi kuwa ataingia tena kwenye orodha ya makipa wanaowania tuzo hiyo na huenda akaichukua kwa mara ya tatu. Nani anajua kitakachotokea?

Razack Abalora- Azam

Ni kipa namba moja wa Azam ambaye alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea WAFA ya Ghana.

Abalora alitua hapo mara tu baada ya kuondoka kwa Manula aliyeichezea klabu hiyo kwa mafanikio.

Abalora amecheza mechi 20 kati ya 25 ambazo Azam imecheza mpaka sasa msimu huu. Kati ya mechi alizozikosa, tatu zilitokana na adhabu ya kufungiwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.

Katika mechi 20 ambazo kipa huyo amecheza, ameruhusu mabao 14 katika mechi tisa wakati katika mechi 11, ameweza kutoka salama dakika zote tisini bila nyavu zake kuguswa.

Youthe Rostand-Yanga

Yanga mara baada ya kumaliza msimu uliopita na kuachana na makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ ilimsajili Youthe Rostand kutoka African Lyon ambayo ilishuka na kwenda Ligi Daraja la Kwanza.

Rostand ameweza kuwa kipa namba moja katika kikosi Yanga licha ya ukweli kwamba amekuwa na makosa mengi katika baadhi ya mechi.

Katika mechi 23, ambazo Yanga imecheza mpaka sasa, Rostand ameruhusu mabao 13. Habari njema ni kwamba naye amecheza mechi 11 bila kuruhusu bao msimu huu, japokuwa si mfululizo.

Benedit Tinocco- Mtibwa

Kipa wa Mtibwa Sugar, Benedict Tinocco, amekuwa na msimu mzuri kwani amecheza mechi 23 na kuruhusu mabao 18 tu. Mabao hayo amefungwa kwenye mechi 13 wakati nyingine 10 zilimalizika bila wavu wake kutikiswa.

Kiwango cha kipa huyo msimu huu kimeibeba timu yake na kuiweka kwenye daraja la juu. Tangu ameanza kucheza Ligi Kuu hajawahi kucheza kwa kiwango cha juu kama afanyavyo msimu huu.

Kabla ya kutua Mtibwa Sugar, alikuwa akisugua benchi Yanga.

Agathony Anthony-Lipuli

Kipa huyu ameidakia Lipuli katika mechi zote 26 ambazo wameshacheza na amefungwa mabao 21. Mabao hayo amefungwa katika mechi 17 huku nyingine tisa akizimaliza bila kuruhusu bao. Agathony amekuwa miongoni mwa makipa wazuri ligi kuu msimu huu.

Kama ataweza kucheza katika kiwango kama ambacho ameonesha, basi mwishoni mwa msimu anaweza kuingia katika orodha ya makipa ambao watawania tuzo hiyo kutokana na rekodi yake nzuri ambayo anayo msimu huu.

Aaron Kalambo-Prisons

Huyu ni kipa wa Tanzania Prisons ambayo ipo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Kalambo amekuwa na uwezo mkubwa wa kuokoa michomo mingi ya wazi na pengine asingekuwepo katika timu hiyo, hadithi ingekuwa tofauti kwa maafande hao.

Kalambo ameruhusu mabao 17 katika mechi 16 huku katika michezo mingine tisa akiibuka shujaa zaidi kwani timu yake iliondoka uwanjani bila kuruhusu bao lolote.

Huwezi kuyatenganisha mafanikio ya Prisons msimu huu na Kalambo, kwani pamoja na timu hiyo kuwa na safu imara ya ushambuliaji, safu ya ulinzi chini ya jemedari huyo imekuwa imara zaidi.

Prisons ni timu ya nne kuruhusu mabao machache msimu huu, imetanguliwa na Simba, Yanga na Azam tu.

Juma Kaseja-Kagera

Wanasema ng’ombe hazeeki maini. Baada ya kulitawala soka la Tanzania kwa zaidi ya miaka 15, Kaseja bado ameendelea kuwa kipa wa kiwango cha juu.

Msimu huu ameendelea kuichezea Kagera Sugar aliyojiunga nayo msimu uliopita ambapo aliingia katika Tatu Bora ya makipa ambao wanawania tuzo hiyo iliyoenda kwa Manula.

Msimu huu hajafanya vizuri sana kwani ameruhusu mabao 25 katika wavu wake, lakini kiwango chake kwenye baadhi ya mechi kinatosha kumweka kwenye orodha hii. Timu yake ipo kwenye kiwango kibovu lakini Kaseja ameendelea kuwa imara