Juma awatuliza mashabiki Stand United

Muktasari:

Stand United inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa

Mwanza. Baada ya kutua Stand United, mshambuliaji Abdalah Juma amewatuliza mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia  kamwe hawawezi kushuka daraja msimu huu.

Stand United iko katika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi 11.

Mshambuliaji huyo aliyewahi kutamba Simba na Mbeya City alisema watapambana kuhakikisha wanatoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Juma aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuipa sapoti ambapo amesema kamwe hawawezi kushuka daraja msimu ujao kwani watapambana kuhakikisha kila mechi wanapata matokeo mazuri.

“Ukingalia hata kwenye msimamo hatujapishana pointi nyingi kikubwa ni sisi wachezaji kupambana uwanjani ili kuweza kujinasua kutoka  mkiani,” alisema Juma.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo,Agustino Malindi alisema kwa sasa wako katika mazoezi makali ambapo amesema pamoja na mambo mengine  wao wamejikita zaidi kwenye safu ya ushambuliaji.

 “Hivi sasa tunatumia muda mwingi kuboresha safu ya ushambuliaji  ambayo katika mechi 11 tulizocheza tumefunga mabao matatu pekee ndio maana tumewasajili kina Abdalah Juma waongeze nguvu,” alisema Malindi.