Julio aishangaa TFF na mapro 10

Muktasari:

  • Rais wa TFF, Wallece Karia alitangaza ongezeko hilo kutoka wachezaji saba hadi 10 kuanzia msimu ujao ambapo zinaruhusiwa kusajili katika usajili  huu unaoendelea.

KOCHA Mkuu wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo 'Julio' ameshangwa na uamuzi uliotolewa hivi karibu na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuruhusu klabu kusajili wachezaji 10 wa kigeni na wanaruhusiwa kuwatumia wote wa wakati mmoja akitamka kuwa hatma ya Taifa ni mbaya.
Rais wa TFF, Wallece Karia alitangaza ongezeko hilo kutoka wachezaji saba hadi 10 kuanzia msimu ujao ambapo zinaruhusiwa kusajili katika usajili  huu unaoendelea.
Akizungumza na Mwanaspoti, Julio alisema licha ya uwepo wa wachezaji wengi wa kigeni ambao wataongeza changamoto kwa wazawa lakini haungi mkono ongezeko hilo ili kunusuru viwango vya wachezaji wa ndani ambao ndio wanawajibika kutumikia timu za Taifa.
“Sawa kanuni mpya ya kuongezeka kwa wachezaji wa kigeni inaweza kuwa na maana kwa jinsi walivyoipitisha walivyohisi na pia itaongeza changamoto kwa wachezaji wazawa lakini bado sijaunga mkono uamuzi huo kwa sababu utaathiri soka letu na hata timu zetu za taifa,” alisema Julio
Julio aliongeza kuwa wachezaji wazawa wanapaswa kuwa sehemu ya lawama hizi za kusababisha wachezaji wa kigeni kuongezeka kwa sababu wachezaji wengi wanashindwa kutambua wajibu wao kuhakikisha wanajituma ipasavyo ili timu zao zisihangaike kutafuta wachezaji wa nje.