Julio ajingamba kimtindo

Muktasari:

  • Uamuzi wake wa kurudi kufundisha soka ni kamari katika kutimiza ndoto yake ya kuipandisha timu hiyo.

 

Furaha ya ushindi mnono wa mabao 3-1 iliyoupata timu yake Dodoma FC ugenini dhidi ya Transit Camp umezidi kumpa kichwa kocha Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’.

Julio amefichua uamuzi aliofanya mwaka jana alipotangaza kujiuzulu kufundisha soka ulikuwa ni kweli na hakutarajia kurejea uwanjani kuwa kocha lakini kitendo cha kukubali kuinoa timu aliyonayo hivi sasa ni zaidi ya kamari.

Julio alisema licha ya ukweli kwamba alishawahi kuzipandisha daraja timu kadhaa huko nyuma, lakini uamuzi wake wa kurudi kufundisha timu hiyo ulikuwa mgumu.

“Kama unakumbuka nilijiweka pembeni kufundisha soka kutokana na sababu mbalimbali ila kiukweli uamuzi wa kurudi kufundisha timu ndio mgumu zaidi tena kukubali kuinoa timu yenye lengo la kwenda Ligi Kuu hakika ni zaidi ya kamari ambayo lazima niishinde,”alisema Julio.

Katika hatua nyingine kocha huyo wa zamani wa Simba SC alisema ushindi wa bao 3-1 iliyoupata  ugenini dhidi ya Transit Camp ni moja ya dalili za kufanikiwa kushinda kamari aliyoicheza, lakini bado ana kazi ya kuifanya.

“Ushindi tulioupata dhidi ya Transit Camp ndio mkubwa tangu tumeanza ligi yetu ikizingatiwa tumecheza ugenini ambapo kushinda ugenini kwa bao hizo ni ngumu ila iliwezekana kulingana na ubora wa timu yangu pia bado nina kazi ya ziada kuhakikisha timu inaenda ligi kuu.”o

Baada ya ushindi huo, Dodoma FC inaongoza Kundi C ikiwa na pointi 15 ikifuatiwa na Alliance ya Mwanza yenye pointi 13, huku Biashara Mara ikiwa na point inane katika nafasi ya tatu.