Wadau wahamasishwa kumsaidia Chama

Muktasari:

  • Mziba ametoa wito kwa wachezaji wa zamani kusaidiana kwenye matatizo kwani Jogoo alikuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga enzi zake.

BEKI  wa zamani wa Yanga, Athuman Juma Chama 'Jogoo'amelazwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili katika hodi namba tano ya Mwaisela kutokana na kusumbuliwa na  ugonjwa wa kupooza.

Kwa mujibu wa staa wa zamani wa timu hiyo, Abel Mziba alisema Jogoo alikuwa anaendelea vizuri lakini ghafla hali hiyo imejirudia.

Amesema: "Alikuwa anaendelea na matibabu, ghafla alijisikia mwili wake unachoka kama vile mtu aliyefanya mazoezi magumu yakamnyong'onyesha mwili, ila tayari ameanza matibabu."

Mziba alitoa wito kwa wachezaji wa zamani kusaidiana kwenye matatizo kwani Jogoo alikuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga enzi zake.

"Shujaa anaumwa, kibinadamu lazima tujiongeze kwamba mwenzetu anapokuwa kitandani hawezi kuingiza kitu chochote cha kuendesha maisha ya familia yake, tumsaidie tutapata thawabu kwa Mungu,"alisema.

"Hata kwa wachezaji wa sasa kama wanapata nafasi waende kumtembelea, nadhani anaweza akafarijika zaidi."