Jiji la Dodoma mwenyeji wa Umisseta na Umitashumta mwakani

Muktasari:

Majaliwa alitangaza uamuzi huo wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo leo kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza.

Mwanza. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amelitangaza Jiji la Dodoma kuwa mwenyeji michezo ya Umisseta na Umitashumta mwakani.

Majaliwa alitangaza uamuzi huo wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo leo kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza.

"Tunashukuru Mkoa wa Mwanza kwa kuwa mwenyeji wetu kwa miaka mitatu mfululizo na tumefurahi kwa huduma zao, niseme mwakani Dodoma ndio watakuwa wenyeji," amesema Majaliwa.

Naibu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema kuwa wao kama Wizara wanatambua umuhimu wa Michezo hiyo kwani imekuwa na matokeo mazuri.

"Tunajivunia uwepo wa Michezo hii sisi kama Wizara, kwani imekuwa na matokeo mazuri ikizingatiwa kwamba ni juzi tu tumewapokea vijana wetu wa Serengeti Boys waliotoka katika mashindano ya Cecafa kwa ushindi," amesema Shonza.

Michezo ya Umisseta ilianza kurindima tangu Juni 4 katika viwanja vya Nsumba na Butimba ikishirikisha mikoa 28 ya Tanzania Bara na Visiwani, huku ile ya Umitashumta itaanza rasmi Juni 16 kwa kuwashirikisha wanamichezo 3,172 kutoka Mikoa 28 ya Tanzania na Zanzibar.