Jezi ya Mzamiru yatua hadi Ikulu

Muktasari:

  • Namba 19 iliyokuwa kwenye jezi hiyo nyeupe ni jumla ya mataji iliyotwaa Simba, lakini pia ndiye jezi anayoivaa kiungo huyo fundi, kitu kilichomfanya Mzamiru kuchekelea akiamini ni mchezaji mwenye bahati ya aina yake.

KAMA kuna mchezaji mwenye furaha Msimbazi kwa sasa ni Mzamiru Yassin. Unajua kwanini? Juzi Jumapili, Rais wa klabu ya Simba, Abdallah Salim ‘Try Again’ alimkabidhi Waziri wa Habari Michezo na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe jezi yenye namba 19 ili amfikishie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli.

Namba 19 iliyokuwa kwenye jezi hiyo nyeupe ni jumla ya mataji iliyotwaa Simba, lakini pia ndiye jezi anayoivaa kiungo huyo fundi, kitu kilichomfanya Mzamiru kuchekelea akiamini ni mchezaji mwenye bahati ya aina yake.

“Ninachojisikia faraja ni kuona Simba imefikia idadi ya mataji ambayo ni sawa na jezi niliyokuwa naitumia katika Ligi Kuu. Ajabu zaidi amekabidhiwa Rais Magufuli jezi kama yangu, naamini nitafika mbali zaidi katika soka,” alisema Mzamiru.

Alisisitiza hakuna mchezaji anayechukia kuona jezi anayoitumia ndio imeangukia historia kubwa ambayo haitasahaulika katika vizazi ambavyo vitafuata nyuma yao.

Mbali na furaha ya jezi yake kutumika kama zawadi kwa Rais na idadi ya ubingwa waliochukua Simba, alisema tayari wameanza mazungumzo ya hapa na pale na mabosi wake ya kuona ni namna gani wafikie makubaliano ya kumbakiza klabuni hapo.

“Ni kweli nimeanza mazungumzo nao, lakini bado hatujafikia mwafaka kama ninaweza kubaki ama kutimka, nasubiri tumalize mechi na Majimaji nadhani hapo ndipo jibu kamili litapatikana,” alisema.