Jeuri ya kocha wa Ruvu Shooting chanzo hiki hapa

MAANDALIZI  ya   Ruvu Shooting  yamempa jeuri kocha wa kikosi hicho, Abdulmutik Haji ambaye anaamini wanauwezo  wa kumaliza ndani ya nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita wa 2018/19, Ruvu Shooting yenye maskani yake Pwani imaliza kwenye nafasi ya nane wakiwa na pointi 38 sawa na Lipuli ambao walimaliza kwenye nafasi ya saba kutokana na utofauti wa mabao ya kushinda na kufungwa.

 Haji ameyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa ziara ya siku tatu ambayo wameifanya Makonga wilayani Newala mkoani Mtwara.

 "Vijana wako tayari kuanza msimu mpya wa ligi, tumecheza mechi nne ambazo zimetupa mwanga kwa kukiboresha kikosi, msimu uliopita hatukuwa na mwanzo mzuri lakini kwa sasa itakuwa tofauti.

 " Lengo ni kumaliza kwenye nafasi nne za juu, mshabiki wetu wategee hilo na pia tunajivunia kama klabu changa nchini kuendelea kupanuka kwa kuwa na mashabiki hata nje ya Pwani," alisema kocha huyo.

 Ruvu Shooting itauanza msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwa kucheza dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mabatini, Agosti 22.

 Hata hivyo, Haji alisema anatarajia kupata mchezo mmoja wa kirafiki kama kipimo chao cha mwisho kabla ya kuanza kwa msimu huo ambao utafunguliwa Agosti 18 kwa mchezo wa hisani kati ya Simba na Mtibwa Sugar.

 Miongoni mwa wachezaji wapya walioongezwa kwenye kikosi cha Ruvu Shooting ni washambuliaji, Abdallah kilala  na Mohammed Hasheem  'Mdoe'.