Jeuri ya MO haipoi kabisa Simba

Muktasari:

Tiketi ya kimataifa kwa michuano ya Afrika mwakani imetua kibabe kwa Wekundu hao, lakini nyuma ya jeuri hiyo yote ni bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji ambaye sasa ndiye atakayekuwa mmiliki wa klabu hiyo.

HUU ni mwaka wa Simba. Kama unabisha ni wewe tu. Kwani kama ni Kombe la Ligi Kuu Bara tayari limeshatua Msimbazi.

Tiketi ya kimataifa kwa michuano ya Afrika mwakani imetua kibabe kwa Wekundu hao, lakini nyuma ya jeuri hiyo yote ni bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji ambaye sasa ndiye atakayekuwa mmiliki wa klabu hiyo.

MO Dewji amekuwa akimwaga fedha kuhakikisha Simba msimu huu inatisha na sasa anaenda kupata baraka za kuwa mmiliki wa hisa za asilimia 49, ili mambo yawe moto zaidi.

Ipo hivi.

Kama hujui, jana Jumapili Wanachama wa Simba walikutana kwenye Mkutano Mkuu wa Dharura na kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya inayoifanya klabu yao sasa kuwa Kampuni, MO Dewji akimiliki kwa asilimia 49, huku zilizobaki zitakuwa za wanachama, huku vyeo kadhaa vikiondolewa kuifanya Simba kuzaliwa upya.

Wanachama zaidi ya 900 waliokutana kwenye mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam umeridhia mabadiliko ya katiba ndani ya Simba na sasa itaendeshwa kwa mfumo wa kampuni ambao utamfanya kila mwanachama awe mwanahisa wa kampuni hiyo.

Mabadiliko hayo yatamfanya kila mwanachama wa Simba kupata gawio la fedha kulingana na faida itakayozalishwa na klabu hiyo kupitia vyanzo mbalimbali kila mwaka.

HADI WARITHI WAMO

Mbali na hilo, kupitia mabadiliko hayo mwanachama wa Simba atakuwa na nafasi ya warithi wake kunufaika pindi atakapofariki dunia na hisa zake zitauzwa na fedha zitakazopatikana kupewa msimamizi wa mirathi ya mwanachama aliyefariki dunia. Wakati wanachama wa Simba wakijadili Rasimu ya Katiba ya kuifanya klabu yao iwe kampuni na kuzika mfumo wake wa uendeshaji wa sasa, kabla mambo hayajakaa sawa, uongozi wake umeahidi neema kubwa ya ndani ya uwanja kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

Neema hizo ni kuimarisha kikosi kwa kusajili mastaa wanaotamba ndani na nje ya nchi sambamba na kuanza ujenzi wa miundombinu ya klabu. MSIKIE TRY AGAIN “Nawaambieni Wanasimba, baada ya mabadiliko haya Simba itakuwa na mafanikio makubwa ya ndani na nje ya uwanja.

Tutahakikisha tunaimarisha kikosi chetu kwa kumsajili mchezaji yeyote mzuri tutakayemhitaji kwa gharama yoyote ile ya fedha ambayo itahitajika. Kuanzia msimu ujao tutaanza kutumia uwanja wetu kwenye mechi mbalimbali za timu yetu,” alisema Kaimu Rais wa Simba, Dk Salim Abdallah ‘Try Again’ katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo.

Kauli hiyo ya Try Again ilionekana kupokelewa kwa furaha na wanachama wa Simba waliojitokeza kwenye mkutano huo wa kujadili mabadiliko hayo.

Kaimu rais huyo alisema klabu hiyo inakwenda kuwa na nguvu kubwa kiuchumi itakayoifanya ipate iweze kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi ambayo yataanza kuonekana hivi karibuni kupitia uendeshaji huo wa mfumo wa kampuni. Mabosi wa Simba pia waligusia kauli ya Rais John Magufuli ya kutaka wakachukue ubingwa wa Afrika, wanaichukulia kama amri na wataitekeleza kwa namna watakavyojipanga. Rais Magufuli aliitoa kauli hiyo juzi katika hotuba yake kabla ya kuikabidhi Simba taji lao la Ligi Kuu Bara, walipovaana na Kagera Sugar na kulala bao 1-0.

MCHONGO ULIVYO

Awali akitoa ufafanuzi wa kina kwa wanachama zaidi ya 900 waliohudhuria mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Simba, Wakili Msomi Evodius Mtawala alisema Asilimia 51 za hisa za klabu zitamilikiwa na wanachama na kusimamiwa na Baraza la Wadhamini. Wakili Mtawala alitoa ufafanuzi kuwa ndani ya kampuni hiyo ya Simba kutakuwa na kampuni haitojihusisha na biashara yoyote itakayofanywa na Simba Kampuni na badala yake itahusika na usimamizi wa hisa za wanachama tu ambayo itajulikana kwa jina la Simba Sports Club Holding Company. Alisema katika katiba ambayo itaendesha Simba kwa mfumo wa Kampuni, kuna kipengele cha kuongeza idadi ya wajumbe wa kuwasimamia wanachama kwenye bodi kutoka saba hadi nane lengo likiwa ni kutoa fursa ya kuwepo angalau mjumbe wa bodi wa jinsia ya kike. Hata hivyo, alisema kipengele hicho kitapitishwa kwa ruhusa ya mkutano mkuu ambao baadaye ulipitisha kipengele hicho kwa wingi wa kura ya ndio baada ya Kaimu Rais, Dokta Salim Abdallah kuomba ridhaa yao.

DK MWAKYEMBE

Akizungumza kwa niaba ya Serikali katika mkutano huo wa jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dokta Harrison Mwakyembe alisema Serikali imekubali mabadiliko ya Simba kwa sababu yanaleta tija kwa maendeleo ya michezo nchini. “Serikali inaamini hiki kilichofanyika sio tu kitaisaidia Simba bali hata timu nyingine.

Serikali inaunga mkono uwekezaji katika michezo lakini tuliona ni vyema tuweke kanuni na sheria ili uwekezaji huo usije kuleta matatizo. Wakati suala hili linaanza, changamoto kubwa ilikuwa ni huo uwekezaji ufanyike kwa mfumo gani kwani kila mtu alikuja na mawazo yake.

Sisi tulichokifanya ni tulikusanya maoni hayo na tukaona mfumo huu wa wanachama kumiliki asilimia 51 na mwekezaji kuwa na 49 ndio unafaa zaidi,” alifafanua Waziri Mwakyembe katika hotuba yake.