VIDEO-Jebby aliyeimba Swahiba na Afande Sele afariki dunia

Muktasari:

  • Khamis amesema, Jebby alianza kuugua tangu Januari mwaka huu na alianza matibabu kwanza mkoani Iringa,  hali ilivyokuwa mbaya alimchukua kwenda kumuuguza Dodoma.

MSANII Jenedy Omari’Jebby’, aliyetesa na kibao cha Swahiba amefariki dunia leo majira ya saa tisa mchana akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Generali Mjini Dodoma.

Taarifa hizo zimethibitishwa na mdogo wake, Khamisi Omary, aliyezungumza na MCL Digital, leo Jumapili kwa njia ya simu.

Khamis amesema, ndugu yake huyo alianza kuugua tangu Januari mwaka huu na alianza kwanza matibabu mkoani Iringa, hali ilivyokuwa mbaya alimchukua kwenda kumuuguza Dodoma.

Amesema, ugonjwa mkubwa uliokuwa ukimsumbua ni kupungukiwa damu na kuvimba bandama na ndio anaamini umechukua maisha yake.

Kwa mujibu wa mdogo wake huyo amesema, shughuli za mazishi zitafanyika nyumbani kwa babu yake Area C mjini Dodoma na maziko yatakuwa saa kumi jioni.

Kwa upande wa msanii Afande Sele, amesema amesikitishwa na msiba huo kwani mwezi mmoja uliopita Jebby alimpigia simu na kumueleza nia yake ya kutaka wafanye video ya wimbo wa Swahiba.

“Yaani ni mwezi tu umepita Jebby alinipigia simu na kuniambia anataka tufanye video ya wimbo wa swahiba, kwa kuwa ameona wasanii wengi wanazifanyia video nyimbo zao za zamani, nasikitika hatujalitekeleza hilo, leo napata taarifa kuwa amefariki,”amesema Afande Sele.