Jamaa wanajua kuwatesa waingereza

Muktasari:

Taarifa mbaya ni kwamba timu hizo zitakutana zenyewe kwa zenyewe katika hatua hiyo jambo litakalofanya ibaki timu moja tu katika hatua ya nusu fainali, huku Hispania ikiwa na timu tatu, Real Madrid, Barcelona na Sevilla, ambazo zote zimepangiwa wapinzani tofauti wakipangwa kucheza dhidi ya Juventus, AS Roma na Bayern Munich kwa kufuata mtiririko ulivyo.

LONDON, ENGLAND. LIGI ya Mabingwa Ulaya imeshafika hatua ya robo fainali na kuna timu mbili za England zilizofanikiwa kutinga hatua hiyo, Liverpool na Manchester City.

Taarifa mbaya ni kwamba timu hizo zitakutana zenyewe kwa zenyewe katika hatua hiyo jambo litakalofanya ibaki timu moja tu katika hatua ya nusu fainali, huku Hispania ikiwa na timu tatu, Real Madrid, Barcelona na Sevilla, ambazo zote zimepangiwa wapinzani tofauti wakipangwa kucheza dhidi ya Juventus, AS Roma na Bayern Munich kwa kufuata mtiririko ulivyo.

Lakini, kwa timu za England pengine zitafurahia ratiba hiyo baada ya huko kwenye timu nyingine kuwapo na mastaa hao ambao huwa hawachoki kufunga mabao dhidi ya timu za Ligi ya Mabingwa Ulaya wanapokutana nazo kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Thomas Muller wa Bayern Munich, Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Lionel Messi wa Barcelona, wote hao ni hatari kwa kupasia nyavu wanapocheza dhidi ya Waingereza.

Makala haya yanahusu wachezaji waliozifunga mara nyingi timu za Ligi Kuu England walipomenyana nazo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

5. Samuel Etoo - mabao 8

Gwiji wa Cameroon, Samuel Eto’o ni mchezaji kutoka Afrika aliyebeba mataji kibao kwenye soka lake alilocheza huko Ulaya. Staa huyo alipita kwenye timu za maana tu, Barcelona, Inter Milan, Chelsea, Everton na sasa yupo Uturuki. Wakati wake wa uchezaji alibeba mataji mengi tu kwenye ngazi ya klabu na timu ya taifa, hakubeba tu Kombe la Dunia.

Kuhusu kuzitesa timu za Ligi Kuu England alipokutana nazo kwenye michuano ya Ulaya, hilo halina mjadala baada ya fowadi huyo kufunga mabao manane dhidi ya timu hiyo.

4. Rivaldo - mabao 8

Staa wa Kibrazili na ni mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or. Rivaldo alienjoi sana alipokuwa akicheza dhidi ya timu za Kingereza. Mkali huyo wa zamani wa Barcelona alifunga mabao manane dhidi ya timu za Ligi Kuu England alizokutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kiukweli, Rivaldo alikuwa hauzuili katika enzi zake za uchezaji, hasa pale alipokuwa kwenye ubora wake. Mancheter United ni miongoni mwa timu zilizowahi kukumbana na makali ya kiungo huyo mchezeshaji wakati huo alipokuwa kwenye ubora wake.

3. Thomas Muller - mabao 9

Fowadi wa Bayern Munich, Thomas Muller ni miongoni mwa wachezaji wanaozitesa sana kwa mabao timu za Ligi Kuu England pindi wanapokutana nazo kwenye michuano ya Ulaya. Kinachonekana ni kama vile, Muller anafunga kwa kadri anavyotaka anapomenyana na timu za England kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hachezi sana kwenye eneo la kushambulia, lakini uwezo wake wa kupasia nyavu hauna tofauti kabisa na ule aliokuwa nao Frank Lampard. Muller amefunga mara tisa dhidi ya timu za England huku Arsenal akiwa amewaonea mara nyingi zaidi.

2. Cristiano Ronaldo - mabao 11

Supastaa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anashikilia rekodi ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mwanasoka huyo bora mara tano duniani anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mara nyingi dhidi ya timu za England walipokutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ronaldo amefunga dhidi ya Liverpool, Manchester City, Tottenham Hotspurs na hata dhidi ya timu yake ya zamani ya Manchester United. Kwa ujumla wake, fowadi huyo wa Ureno amefunga mara 11 dhidi ya timu za Ligi Kuu England alizokutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

1. Lionel Messi - mabao 20

Staa wa Barcelona, Lionel Messi alisubiri kwa mechi tisa kufunga bao lake la kwanza dhidi ya Chelsea baada ya kufanya hivyo katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika Stamford Bridge.

Kwenye mechi ya marudiano iliyofanyika Nou Camp, Messi aliwapiga mbili Chelsea na hivyo sasa ana mabao matatu dhidi ya timu hiyo. Hiyo ndiyo timu ya England iliyokuwa ikimsumbua Messi kuifunga kati ya zile alizowahi kukutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa ujumla, Messi sasa amefunga mabao 20 dhidi ya timu za England, Arsenal akionea zaidi, lakini pia Manchester United na Manchester City zimeshawahi kukutana na machungu ya kufungwa na staa huyo.