JKT Tanzania yakalia usukani wa Ligi Kuu

Muktasari:

JKT Tanzania imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza

Mwanza. JKT Tanzania imekalia usukani wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Mbao FC kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ushindi huo unaifanya JKT Tanzania kufikisha pointi nane kileleni huku ikifuatiwa kwa karibu na Azam, Mbao na Simba zenye pointi saba kila mmoja.

Shujaa wa JKT Tanzania alikuwa Ahmed Ally aliyefunga bao hilo pekee kwa mkwaju wa penalty katika dakika za nyongeza baada ya Hassan Materema kuangushwa eneo la hatari na Peter Mwangosi wa Mbao FC.

Katika mchezo huo wa raundi ya nne kwa timu hizo uliopigwa katika uwanja wa CCM Kirumba, JKT walionekana kuwa na uchu zaidi wa kuhitaji mabao ya haraka lakini ubutu wa safu ya ushambuliaji umeweza kuwagharimu.

Nafasi takribani tatu za washambuliaji Hassan Materema na Mohammed Simba ambao walionekana kuelewana kwa kupasiana pasi lakini walishindwa kufunga mabao.

Wenyeji Mbao watajilaumu kwa nafasi mbili takatifu ambazo nyota wao, Pastory Athanas akiwa ndani ya 18 alishindwa kufunga.

Mbeya: Tanzania Prison imeshindwa kuutumia vyema uwanja wake was nyumba baada ya kulazimishwa sare mabao 2-2 na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Prison ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Hassan Kapalata dakika 74 kwa shuti kali nje ya 18, Ruvu Shooting ilisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penalti dakika 79, iliyofungwa na Hamid Muha kabla Ayub Kitara kufunga bao la pili.

Wenyeji Prison iliamka na kusawazisha kupitia kwa Salum Kimenya.

Mara: Biashara United ikicheza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima imelazimishwa suluhu na Kagera Sugar katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu bara kufanyika kwenye Uwanja wa Karume, Mara.

Biashara United ikicheza mbele ya mashabiki wake ilianza mchezo huo kwa kasi lakini washambuliaji wake walishindwa kuipenya ngome ya Kagera Sugar.

Katika mchezo mwingine Mjini Iringa, wenyeji Lipuli imelazimishwa suluhu na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

KMC ikiwa nyumbani Uwanja wa Uhuru ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Singida United shukrani kwa bao la Habib Kiyombo.