JKT Ruvu yazitolea nuksi klabu za Bongo, yazindua uwanja wake

Muktasari:

Uwanja huo ambao ujenzi wake wa awali umekamilika huku ukigharimu kiasi cha Shilingi 25 milioni, utatumiwa na timu ya JKT Ruvu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) leo limezindua uwanja wa soka kwenye kambi yake ya Mbweni ambao umepewa jina la Meja Jenerali Michael Joseph Isamuhyo ambaye ni mkuu wa jeshi hilo.

Uwanja huo ambao ujenzi wake wa awali umekamilika huku ukigharimu kiasi cha Shilingi 25 milioni, utatumiwa na timu ya JKT Ruvu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Mwenyekiti wa timu ya JKT Ruvu, Luteni Kanali Hassan Mabena alisema uamuzi wa jeshi kujenga uwanja huo ni kuendeleza juhudi zake za kuinua sekta ya michezo.

"Malengo yetu ni kujenga taasisi ya kudumu ya michezo katika eneo hili. Uwanja huu sio kwamba utatumika na JKT Ruvu tu bali upo kwa ajili ya Watanzania.

Tunatarajia baada ya kumalizika kwa michezo ya ligi daraja la kwanza tutaanza ujenzi wa majukwaa kama mchoro wa ujenzi unavyoonyesha ambapo tunatarajia utaingiza mashabiki 15,000," alisema Luteni Kanali Mabena.

Mjumbe wa kamati ya ufundi ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, Ally Mayay alipongeza uamuzi wa JKT kujenga uwanja.

"Katika sheria 17 za soka, ya kwanza inaelezea masuala ya uwanja hivyo juhudi zozote zinazofanyika katika utengenezaji na uboreshaji wa miundombinu lazima zipongezwe," alisema Mayay