Ishu ya udhamini Ligi Kuu

WAKATI Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) ikitangaza kutopatikana kwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo msimu ujao, hali imezidi kuwa tete na kuziweka klabu katika mazingira magumu ya kujiendesha na kumudu gharama maandalizi.

Kupitia barua iliyoandikwa na TPLB kwenda kwa klabu za ligi hiyo na kauli ya Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Wallace Karia, taasisi hizo zimethibitisha ligi itaendelea kupata sapoti ya wadhamini washiriki ambao ni kampuni ya Azam Media na Benki ya KCB.

“Ligi Kuu kwa msimu wa 2018/2019 hadi sasa ina wadhamini wadogo wawili tu. Wadhamini hao ni Azam Pay TV ambao wana haki za matangazo na benki rasmi ya Ligi Kuu (KCB Tanzania) ambao ni wadhamini wenza,” inasema sehemu ya barua hiyo ya TPLB kwenda kwa klabu 20 shiriki za Ligi Kuu.

Kupitia udhamini huo kila klabu ya Ligi Kuu itapata kiasi cha Shi 177 milioni kwa msimu mzima ambapo Sh162 milioni ni fedha kutoka Azam Pay TV na Sh15 milioni kutoka Benki ya KCB Tanzania.

Lakini tofauti na hapo awali wakati Vodacom ilipokuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, mbali ya fedha pia walikuwa wakitoa vifaa kwa klabu, waamuzi sambamba na kutoa zawadi kwa washindi, hivyo kukosekana kwao ni balaa kubwa.

Mbali ya vifaa hivyo, Vodacom ilikuwa ikitoa kitita cha takribani Sh2.3 bilioni kwa mwaka, ambapo kila klabu ilikuwa inajichotea takribani Sh80 milioni kwa msimu huku fedha nyingine zikitumika kulipa waamuzi na maofisa wanaosimamia mechi.

Tathmini ya Mwanaspoti imebaini kuwa maisha ya klabu za Ligi Kuu huenda yakawa magumu zaidi kutokana na idadi kubwa kutokuwa na wadhamini binafsi sambamba na vyanzo imara vya mapato.

Kiasi cha Sh177 milioni ambacho kila timu itapata ni kidogo kulinganisha na mahitaji ya uendeshaji wa klabu kwenye Ligi Kuu tofauti na zamani ambapo, kutokana na fedha na vifaa ambavyo Vodacom ilikuwa inatoa, angalau klabu ziliweza kupunguza makali ya gharama za uendeshaji.

Kiasi cha Sh162 milioni kutoka Azam Pay TV kikigawanywa kwa awamu nne ambazo kila moja ina miezi miwili kama utaratibu ulivyo, maana yake kila klabu itapata Sh40.5 milioni.

Kiasi hicho cha fedha ni kidogo pungufu ya robo ya bajeti za uendeshaji wa klabu kubwa tatu nchini za Yanga, Simba na Azam FC ambazo ndizo zinaongoza kwa matumizi katika kujiendesha kwa mwezi, ambapo kuna kulipa mishahara na huduma nyingine.

Azam FC yenyewe imekuwa ikitumia takribani Sh270 milioni ikiwa ni gharama ya kujiendesha kwa mwezi, wakati Simba inatumia Sh230 milioni huku Yanga ikitajwa kutumia zaidi ya Sh200 milioni.

Kwa hesabu za haraka haraka, kiasi cha Sh40.5 ambacho itakipata kutoka udhamini wa Azam Pay TV na kila cha Sh 7.5 milioni ambacho itakipata kwa awamu mbili kutoka KCB Tanzania, hakitoshi kulipa hata mishahara ya wachezaji saba wa kigeni kwenye timu hizo.

Hali huenda ikawa mbaya zaidi kwa timu ndogo au zile zisizo na wadhamini kwani, ratiba ya ligi huenda ikazifanya baadhi kuishiwa fedha mapema tu hasa ukizingatia uwepo wa kanuni inayoelekeza timu mwenyeji kukusanya mapato yote.

Timu kama Lipuli ambayo itaanzia mkoani Tanga dhidi ya Coastal Union ambako italazimika kutumia kiasi kisichopungua Sh5 milioni kwa usafiri, malazi, chakula na posho kwa wachezaji na baada ya hapo italazimika kutumia takribani Sh10 milioni kwa mechi mbili itakazocheza Dar es Salaam baada ya hapo dhidi ya timu za Simba na JKT Tanzania.

Maana yake hadi Lipuli inarudi Iringa kujiandaa na mechi mbili itakazocheza uwanja wake wa nyumbani, itakuwa imeshateketeza kama Sh15 milioni kwa posho, chakula na usafiri tu kati ya Sh40 ambazo ingetakiwa kutumia kwa awamu ya kwanza ya miezi miwili huku bado ikiwa na mtihani wa kulipa mishahara kikosi chake na benchi la ufundi.

Madenti wapewa shavu

Hali ikiwa bado tete kwenye suala la udhamini, wanafunzi wa shule za sekondari na msingi wamepata shavu la uhakika.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, amesema msimu ujao wa ligi wametoa nafuu ya viingilio kwa wanafunzi ambapo wataingia uwanjani kwa nusu bei.

Amesema kuwa kinachotakiwa kufanyika ni kwa mwanafunzi kuwa na kitambulisho kinachotambulika tu kisha wanapata tiketi kwa nusu bei.

“Tiketi hizi zitakuwa nusu bei kwa pesa ambayo wataingia watu wazima uwanjani, lakini pia watakaa maeneo yale ya viti vya kawaida na si viti maalumu na kama kuna, ambaye atataka mwanaye au mwenyewe kukaa hapo anatakiwa kuwa na tiketi ya eneo hilo,” alisema Wambura na kuongeza hiyo inalenga kuwahamasisha vijana.

WASIKIE VODACOM

Lakini wakati TFF na hata Bodi ya Ligi wakitangaza msimu huu hakuna mdhamini mkuu wa Ligi Kuu, waliokuwa walidhamini Kampuni ya Vodacom wamefichua huenda wakarudi kuidhamini ligi hiyo kivingine.

Mtendaji Mkuu wa Bodi, Boniface Wambura jana aliwaambia wanahabari kuwa, igi itaanza bila mdhamini kwa vile hawajampata baada ya Vodacom kumaliza mkataba.

Mashabiki wengi wa soka wanadhani Vodacom ndio wamejiondoa moja kwa moja kudhamini ligi hiyo, lakini kampuni hiyo imeliambia gazeti hili kwamba bado ipo kwenye mazungumzo na TFF kwa ajili ya kuendelea kudhamini Ligi.

“Vodacom Tanzania tumejidhatiti katika kukuza vipaji vya vijana Tanzania. Hili tumekuwa tukilifanya kupitia programu mbalimbali na michezo. Hii ni pamoja na kudhamini Ligi Kuu tuliyoidhamini kwa zaidi ya miaka saba sasa,” alisema Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Vodacom Tanzania, Nandi Mwiyombella.

“Udhamini huu utaendelea na kwa sasa tunaendelea na majadiliano kati yetu na TFF. Mazungumzo yakikamilika tutakuja na jibu sahihi. Ahsante.”

Hata hivyo taarifa ambazo gazeti hili inazo ni kuwa Vodacom wamepanga kuwa wadhamini wenza tu kwenye ligi hiyo kuanzia msimu ujao badala ya wadhamini wakuu kama ilivyokuwa awali, ikidaiwa kutenga Sh500 milioni za udhamini huo.

Kiasi hicho cha fedha ni kama robo ya fedha yote ambayo walikuwa wakiipa TFF pindi walipokuwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo ambapo walikuwa wanatoa kitita cha Sh2.3 bilioni kwa mwaka. Mbali na fedha hizo, Vodacom pia walikuwa wakitoa vifaa kwa timu pamoja na waamuzi sambamba na kutoa zawadi.