Ilivyokuwa dakika chache kabla ya kifo cha Yasoda ofisini Dar

Muktasari:

Si wana familia, majirani, wala wafanyakazi wenzake waliompokea ofisini muda mfupi jana kabla mauti kumkuta tena akiwa mzima wa afya, wanaoweza kuamini.

NI ngumu kuamini, lakini ndio ukweli ulivyo kwamba, Juliana Yasoda, hatunaye.

Si wana familia, majirani, wala wafanyakazi wenzake waliompokea ofisini muda mfupi jana kabla mauti kumkuta tena akiwa mzima wa afya, wanaoweza kuamini.

Mwanamichezo na kigogo huyo wa michezo nchini, alifariki dunia jana Alhamisi baada ya kudondoka ghafla mara tu alipofika ofisi kwake Wizara ya Elimu jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Elimu, Yasoda alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania katika Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Mmoja wa wafanyakazi wenzake aliyejitambulisha kwa jina moja la Maimuna, alisema Yasoda alifika ofisini akiwa mzima, lakini ghafla alidondoka akiwa ghorofa ya kwanza kuelekea ilipo ofisi yake.

“Alifika ofisini mzima tena akiwa anaendesha gari mwenyewe, alipaki vizuri na kupitia funguo za ofisi yake akiwa mzima tu wala hakuna aliyetarajia kama dakika chache baadaye atapoteza maisha, alipitia kwa katibu mkuu na kumsalimia vizuri kisha kuelekea ofisini kwake,” alisema.

“Akiwa anapanda ngazi alidondoka, alikimbizwa hospitali lakini haikusaidia kwani kule walitueleza tayari ameshafariki, mwili wake umehifadhiwa Muhimbili.”

Akizungumzia taratibu za msiba, Maimuna alisema wanasubiriwa ndugu wa marehemu ambao jana walikuwa njiani kuelekea Dar es Salaam kutoka Dodoma.

Wizarani hapo, Yasoda alikuwa Ofisa wa Idara ya Sekondari.