Ikitokea itakuwa BURUDANI top Six

Muktasari:

Mchezo huo mtamu siku zote umekuwa ukiwaleta mashabiki pamoja na siku zote umekuwa na uwezo mkubwa wa kuwafanya mashabiki hao kufurahia, hasa unapomtazama mchezaji kama Lionel Messi akiwa na mpira miguuni mwake uwanjani.

LONDON, ENGLAND

JUMANNE, Machi 20 ilikuwa Siku ya Furaha duniani. Lakini, kwa shabiki wa soka siku zote anakuwa na sababu milioni za kutasamu.

Mchezo huo mtamu siku zote umekuwa ukiwaleta mashabiki pamoja na siku zote umekuwa na uwezo mkubwa wa kuwafanya mashabiki hao kufurahia, hasa unapomtazama mchezaji kama Lionel Messi akiwa na mpira miguuni mwake uwanjani.

Achana na siku hiyo ya furaha duniani, kwenye timu za Ligi Kuu England kuna matukio hayo kama yakitokea kwenye timu za Top Six basi mashabiki wao watakuwa kwenye furaha kweli kweli bila ya kujali ni siku ya furaha duniani au la.

Man City - Kubeba taji Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kitu gani cha kumpa mtu mwenye karibu kila kitu? Kumfurahisha mtu wa aina hiyo ni kumpa kitu ambacho hana au anachotamani kuwa nacho. Kwa kesi ya Manchester City, wao wameshabeba ubingwa wa Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Kombe la FA na wachezaji mahiri na kocha mahiri pia. Kitu pekee ambacho Man City wanakikosa kwa sasa ni taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kubeba taji hilo kutawatambulisha Man City kuwa rasmi ni klabu kubwa barani Ulaya na itaanza kupewa hadhi kubwa kama inazopewa Man United, Real Madrid, Barcelona, Juventus na Bayern Munich na Liverpool. Msimu huu wametinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na wanachopaswa kufanya ni kuvuka vizingiti vyote na kubeba ubingwa huo. Hilo litafurahisha mashabiki wao.

Man United - Kuacha kupaki basi

Kama kuna kitu kinachowakera mashabiki wa Manchester United kwa sasa basi ni timu yao kuweka mkazo kwenye soka la kukaba zaidi kuliko kushambulia. Mashabiki wa timu hiyo watakuwa kwenye furaha kubwa kama watafanikiwa kucheza soka la kushambulia zaidi na kuwapelekesha wapinzani wao kuliko wao kucheza soka la kujilinda tu, kupaki basi. Mtindo huo wa kubaki pasi ndiyo unaowafanya baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kumchukia Jose Mourinho kwa kuwekeza zaidi kwenye kukaba zaidi ya kwenda mbele kushambulia, staili ambayo ilikuwa ikiwapa furaha na burudani wakati huo walipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Liverpool - Salah akisaini mkataba mpya

Mashabiki wa Liverpool ukikutana nao kwa sasa kila mmoja anakenua tu, kisa Mohamed Salah kuwa kwenye kikosi chao.

Salah anacheza soka la kiwango kubwa sana huko Anfield na kuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo na kuwasahau kabisa Luis Suarez na Philippe Coutinho. Kiwango matata cha mchezaji huyo tayari kumemfanya aanze kuhusishwa na Real Madrid, kwamba wanahitaji saini yake jambo linalowapa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo. Mashabiki wa timu hiyo ya Anfield watakuwa na furaha kubwa kweli kweli kama watamwongezea mkataba wa mrefu staa wao kwani hilo litawaondolea presha ya kumpoteza supastaa wao.

Tottenham - Heung-Min Son kubaki kikosini

Ni ukweli kabisa, mashabiki wa Tottenham Hotspur wana furaha kubwa kwa sasa kutokana na kiwango bora cha staa wao kutoka Korea Kusini, Heung-Min Son. Straika, Harry Kane anaweza kuwa mfungaji mahiri kwenye kikosi, lakini mashabiki wa timu hiyo wameonekana kutokuwa na wasiwasi na fowadi huyo kuwa majeruhi kwa sasa kwa sababu tu wanaye Son, ambaye kwa sasa amekuwa mtamu hadi balaa. Son, ndiye mchezaji anayewapa furaha kubwa mashabiki wa Spurs na itakuwa furaha zaidi kwenye timu yao kama ataendelea kubaki kwenye kikosi chao kwa muda mrefu zaidi asije kubebwa na timu nyingine zinazommezea mate.

Chelsea - Conte kubaki Stamford Bridge

Licha ya msimu huu wa pili kuwa mgumu kwa Mtaliano Antonio Conte kwenye klabu ya Chelsea, mashabiki wa timu hiyo watakuwa na furaha kubwa kama kocha huyo ataendelea kubaki Stamford Bridge. Mashabiki wa Chelsea wanamheshimu sana Conte kutokana na namna alivyowafanya kuwa tishio tena kwenye ligi baada ya mambo kuonekana kutibuka kwa kiasi kikubwa. Conte aliwapa Chelsea ubingwa wa Ligi Kuu England muda mfupi tu baada ya kuichukua timu hiyo ambayo ilionekana kama sasa inaelekea kubomoka zaidi. Stori zinazoelezwa ni kwamba Conte anaweza kuondoka na Luis Enrique anakuja kuchukua mikoba yake kitu ambacho mashabiki wa Chelsea hawakifurahii, kwa sababu wanaamini wapo salama zaidi chini ya Conte.

Arsenal - Wenger akitangaza kung’atuka

Kitu kikubwa kinachosubiriwa na mashabiki wa Arsenal kwa msimu huu ni kama timu yake itabeba taji la Europa League na kisha wakapata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Hilo litawapa furaha. Lakini, furaha yao itakuwa kubwa zaidi kama kocha wao king’ang’anizi, Arsene Wenger atatanga kung’atuka kwenye timu hiyo. Wanachokiamini mashabiki wa Arsenal ni kwamba shida kubwa inayowakwamisha wasifanye vizuri kwenye Ligi Kuu England na kusubiri kwa muda mrefu kuubeba ubingwa wa taji hilo ni kocha Wenger na kama akiondoka, basi jambo hilo litakuwa limewafanya kuwa nna furaha kupitiliza.