Iceland, Argentina zimetuachia somo tujifunze

Thursday October 12 2017

 

KAMA kuna kitu kinachoufanya mchezo wa soka kuwa na mvuto ni namna ulivyo na matokeo ya kustaajabisha.

Siku chache zilizopita mashabiki wa soka duniani kote, wakiwamo wa Tanzania walikuwa na wasiwasi wa kuzishuhudia Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018 zitakazofanyika nchini Russia, bila ya kuwepo kwa Messi wala Argentina.

Hii ilitokana na nafasi waliyokuwa nayo katika msimamo wa mbio za timu za nchi za Amerika Kusini.

Hata hivyo, wakati mashabiki wakijadili namna gani wataelekea kwenye fainali za Russia bila nyota huyo wa Barcelona, Messi juzi aliibeba Argentina mabegani mwake na kuivusha kwenda katika fainali hizo zijazo. Mabao matatu aliyoyafunga dhidi ya Ecuador, imeivusha nchi yake na kufuta zile hesabu labda ingecheza hatua ya mtoano (play-off).

Wakati ukiitafakari Argentina, rejea kwa Iceland, moja ya nchi yenye idadi ndogo ya watu imekata tiketi ya kwenda Russia.

Iceland yenye watu wasiofikia 350,000 waliongoza kundi I ikiziacha solemba nchi za Croatia, Uturuki, Ukraine na Finland na kuwenda moja kwa moja fainali za Russia bila kutarajiwa.

Hii ni mara ya pili katika kipindi kifupi, Iceland ikifanya maajabu, ilianza kwa kufuzu fainali za Kombe la Ulaya zilizopita za 2016 na kutinga robo fainali bila kutarajiwa kuwa kuing’oa England na kukwama mbele ya wanafainali, Ufaransa.

Kilichofanywa na Messi na Argentina yake na Iceland linapaswa kuwa somo kwa wadau wa soka hususan viongozi wanaosimamia mchezo huo, wachezaji na wengine ambao wamekuwa na kiu ya kuona Tanzania ikitimba kimataifa.

Upande mmoja, alichokifanya Messi ni kutaka kuwaonyesha nyota wetu namna gani mchezaji tegemeo anavyopaswa kujitoa kwa ajili ya timu yake, kwani nyota huyo aliamua kuibeba timu yake kwa kila hali na kuivusha salama.

Wangapi miongoni mwa wachezaji wa timu zetu wamekuwa wakijitoa na kuamua matokeo yenye faida kwa timu zao?

Lakini Messi na nyota wengine ambao wamekuwa wakishuhudiwa wakizibeba timu zao wamekuwa wakifanya.

Hivi ndivyo wachezaji wanapaswa kuzipigania timu zao bila kukata tamaa ndani ya dakika 90 za pambano la soka.

Mara ngapi tumekuwa tukishuhudia timu zetu zikikata tamaa au kukatishwa na wadau wa soka kutokana na matokeo iliyonayo na hasa katika kuwania nafasi kama iliyokuwa ikiipigania Argentina dhidi ya wapinzani wao wa ukanda wao?

Lakini kumbe katika soka, pale pasipowezekana huwa kunawezekana iwapo tu wachezaji wakiamua kupambana uwanjani kuzipigania timu zao.

Ni ngumu wachezaji wetu kujilinganisha na mechi katika suala la kipaji na umahiri wake uwanjani, lakini ile roho ya mapambano na uzalendo bado wanaweza kuibeba na kuitumia katika mechi zao na kujitengenezea rekodi zisizofutika.

Inasikitika kuona Tanzania tangu ilipoenda Afcon 1980 haijaweza kurudi tena kwenye michuano hiyo kama ilivyoshindwa kurejea rekodi yao ya kushiriki fainali za kwanza cha Chan 2009 kule Ivory Coast.

Hakuna ubishi Tanzania imejaliwa vipaji vikubwa vya soka, lakini namna ya kuvilea na kuviendeleza vipaji hivyo kwa manufaa ya baadaye ya taifa hayapo, ndio maana tumekuwa tukiishia njiani na kuishia kutafuta visingizio.

Ipo haja ya wadau kwa kushirikiana tukatengeneza ajenda moja ya kuhakikisha kwa mfano fainali za Kombe la Dunia za 2026 ama Afcon 2021 tunakuwepo kwa kuanza maandalizi sasa ya kwenda huko. Inawezekana.

Hata Uganda waliweza kwenda Afcon 2017 baada ya zaidi ya miaka 35 kwa sababu walijiwekea malengo na hata fainali za Dunia wamezikosa kwa kuteleza kidogo, hivyo hata sisi tukiamua tunaweza, muhimu kujipanga tu.

Kubwa zaidi ni wachezaji wetu kujaribu kuvaa ujasiri wa Messi na nyota wengine wanaozipigania nchi zao kwa hali na mali ili kuzipa mafanikio.

Kila mchezaji akiwa na moyo wa kizalendo na kujituma uwanjani, huku viongozi wakitekeleza wajibu wao wa kuandaa mipango yenye malengo ya mbali Tanzania itatisha.