Ibrahimovic, Hazard rekodi tamu kabisa

Muktasari:

  • Kichapo hicho kinaifanya Man United sasa kulazimika kushinda katika mechi yao ya mwisho dhidi ya CSKA Moscow itakayofanyika Old Trafford, Desemba ili kufuzu kwa hatua ya mtoano ya 16 bora baada ya kipigo hicho cha Uswisi kuwatibulia mipango,

CHAMA cha Zlatan Ibrahimovic, Manchester United lilichapwa Moja Bila na FC Basel kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku, lakini hilo halikumzuia staa huyo wa Sweden kuweka rekodi yake katika michuano hiyo.

Kichapo hicho kinaifanya Man United sasa kulazimika kushinda katika mechi yao ya mwisho dhidi ya CSKA Moscow itakayofanyika Old Trafford, Desemba ili kufuzu kwa hatua ya mtoano ya 16 bora baada ya kipigo hicho cha Uswisi kuwatibulia mipango,

Lakini, mechi hiyo iliyomshuhudia Ibrahimovic akicheza kwa dakika 25 zilimfanya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyewahi kuchezea timu saba tofauti kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Timu nyingine alizowahi kuchezea Ibrahimovic kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni PSG, Barcelona, AC Milan, Inter Milan, Juventus na Ajax.

Wakati Ibrahimovic akiweka rekodi hiyo, staa wa Chelsea, Eden Hazard na yeye ameandika ya kwake kwenye michuano hiyo akiwa Mbelgiji aliyefunga mara nyingi zaidi katika mikikimikiki hiyo ya Ulaya. Hazard amefunga mabao manane, moja zaidi ya Wabelgiji wengine, Dries Mertens na Wesley Sonck. Hazard alifunga kwa mkwaju wa penalti katika ushindi wa 4-0 dhidi ya FC Qabarag juzi Jumatano.