VIDEO: Huku Samatta, AliKiba kule Joti, Mpoki unakosaje uhondo huu

Muktasari:

  • Samatta na King Kiba kila mmoja akiwa na timu yake watacheza mchezo huo kwa ajili ya kuchangia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uimarishaji wa miundo mbinu kwenye sekta ya elimu.

Dar es Salaam. Hakuna namna ni Mbwana Samatta na AliKiba kila mmoja ataongoza jeshi lake katika mchezo wa hisani kesho kwenye Uwanja wa Taifa majira ya saa tisa alasiri jijini Dar es Salaam.

Samatta na King Kiba kila mmoja akiwa na timu yake watacheza mchezo huo kwa ajili ya kuchangia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uimarishaji wa miundo mbinu kwenye sekta ya elimu.

Siku chache baada ya kutua nchini akitokea Genk, Samatta ameuzungumzia mchezo huo  kwa kusema asilimia kubwa ya wachezaji wake watakuwepo kasoro wachezaji kadhaa  kutokana na sababu za kimajukumu yao.

“Kuna wachezaji wengine ambao wanaendelea na majukumu kwenye klabu zao hao ni ngumu kuwa nao, lakini karibu wote ambao niliwatangaza watakuwepo. Mputu naye hatokuwepo kutokana na sababu za kifamilia,”alisema Samatta.

King Kiba naye kwa upande wake alithibitisha kikosi chake kuwa fiti kwa kusema hata inyeshe mvua au liwake jua lazima timu Samatta ikione chamoto kwenye mchezo huo.

“Elimu ni sekta muhimu ambayo inauhitaji wa mimi na wewe kujitolea, wapo wanaosoma kwenye mazingira magumu kwa hiyo wadau wa muziki, vijana wapenda maendeleo na wanasoka wote tujitokeze,” alisema King Kiba.

JOTI,  MPOKI HAPATA TOSHA

Maandalizi yameiva kwa wasemaji wa timu hizo mbili, Joti wa timu Samatta na Mpoki wa Kiba wamejipanga kutupiana maneno kwenye mchezo huo wa hisani.

Joti anatamba kuwa kabla ya mchezo wa leo wa hisani ameshawapoteza timu Kiba nje ya uwanja, kilichobaki na kazi kwenda kumalizika uwanjani.

Mpoki amedai kumuangalia Joti anavyochonga kwa kusema mpira hauchezwi mdomoni kama maneno ya shombo hata yeye anayaweza watu watajionea uwanja wa taifa.

TIMU SAMATTA

Juma Kaseja, Kabaly Faraji,  Kelvin Yondan, Nadir Haroub, Athumani Chuji, Haruna Shamte, Mohammed Samatta,  Thomas Ulimwengu, Farid Mussa, Haruna Moshi ‘Boban’, Amri Kiemba, Athuman Machupa, Henry Joseph, Rashid Gumbo, Mrisho Ngassa na Sultan Kaskas.

TIMU ALIKIBA

Shaaban Kado, Gadiel Michael, Paul Nonga, Abdul Kiba, Himid Mao,  Agrey Morris, Ibrahim Ajib, Abdi Kassim, Emmanuel Okwi, Abdi Banda, Saimon Msuva, Shaban Kisiga, Uhuru Seleman na  Ramadhani Chombo.