Huko ni Samatta, Msuva

Mbwana Samatta

HAPA Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji na kule ni Saimon Msuva wa Difaa El Jadida ya kule Morocco. Mastaa hawa leo watakiongoza kikosi cha Taifa Stars kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao, Algeria.

Samatta alitua Algeria Jumatatu akitokea Ubelgiji huku Msuva akifuatia kujiunga na kikosi cha Stars, ambacho mara baada ya kuwasili nchini humo, kimetumia siku mbili kujiandaa.

Stars itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mbele ya Algeria, Novemba 17, 2015 nchini humo kwa mabao 7-0 kwenye mchezo wa pili wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumzia mchezo wa leo, Msuva alisema atashirikiana na wenzake kuhakikisha wanapata matokeo. “Algeria ni nchi kubwa kwenye soka la Afrika, hii itatusaidia kama tukishinda kusogea kwenye viwango vya soka duniani, uwezo wa kuwafunga tunao,” alisema Msuva.

Kocha Salum Mayanga alisema kikosi chake hakitakuwa na mabadiliko ya kimfumo na badala yake zinaweza kubadilika mbinu za uchezaji pekee.

Algeria ipo nafasi 60 kwenye viwango vya FIFA wakati Tanzania ni ya 146. Mchezo huo utaanza saa 2:00 usiku, saa za Afrika Mashariki.