Historia inawabeba

MSHAMBULIAJI John Bocco kwa mara ya kwanza ataingia kwenye Tamasha la Simba Day akiwa nahodha tangu alipokabidhiwa majukumu hayo mwaka jana.

Huenda ingekuwa ni mara ya pili kwa Bocco lakini katika tamasha hilo mwaka jana ambalo lilikuwa la kwanza kwake tangu aliposajiliwa Simba, nahodha wa timu hiyo alikuwa ni Mzimbabwe, Method Mwanjale.

Kuelekea tamasha hilo leo Jumatano, gazeti hili linakuletea orodha ya wachezaji waliopata fursa ya kuvaa kitambaa cha unahodha cha Simba kwenye tamasha la Simba Day.

NICODEMUS NYAGAWA - 2009

Nyagawa anabaki kuwa nahodha wa kwanza kihistoria wa Simba kuiongoza timu hiyo kwenye Tamasha la Simba Day mwaka 2009 ambapo ndipo tamasha hilo lilianzishwa rasmi na klabu hiyo chini ya uongozi wa Hassan Dalali aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo.

Nyagawa aliyekuwa anacheza nafasi ya kiungo, kwa sasa amekuwa akishiriki tamasha hilo kama kocha wa kikosi cha vijana cha Simba akiwa sambamba na mastaa wa zamani wa Simba, Nico Kiondo na Musa Hassan ‘Mgosi’

Mwaka 2010 lilikuwa tamasha la mwisho kwa Nyagawa kuhudumu kama nahodha kwani baada ya msimu wa 2010/2011 alistaafu rasmi kucheza soka na kugeukia ukocha akiwa mmoja wa nyota waliokuwa vipenzi kwenye klabu hiyo. Nyagawa baada ya kustaafu aliwahi kuwa meneja wa kikosi cha Simba.

JUMA KASEJA - 2011

Baada ya Nyagawa kustaafu, kitambaa cha unahodha wa Simba kilitua begani kwa kipa Juma Kaseja ambaye alitambulishwa kwenye tamasha la mwaka 2011 ambalo timu hiyo ilicheza mchezo wa kirafiki na timu ya Victors kutoka Uganda na kuchapwa 1-0. Kaseja aliendelea kuwa nahodha hata tamasha la 2012, ingawa ni kama alikuwa na nuksi na matamasha ya Simba Day akiwa kama nahodha kwani mwaka huo alishuhudia timu yake ikitota mbele ya Nairobi City Stars baada ya kuchapwa mabao 3-1.

Tamasha la mwaka 2012 lilikuwa la mwisho kwa Kaseja kwani baada ya hapo aliachana na Simba.

JOSEPH OWINO - 2013

Kwenye Tamasha la Simba Day mwaka 2013, kitambaa cha unahodha wa Simba kilikuwa begani kwa beki raia wa Uganda, Joseph Owino ambaye kabla ya hapo alishiriki tamasha hilo akiwa mchezaji wa kawaida mwaka 2010.

Owino alishiriki kwa mara ya pili Simba Day akiwa nahodha mwaka 2014 ambalo lilikuwa la mwisho kwake kabla ya kuachana na timu hiyo na kurudi kwao Uganda.

NASSORO MASOUD ‘CHOLLO’ - 2015

Mkongwe Chollo baada ya kushiriki matamasha sita ya nyuma ya Simba Day, awamu hii aliingia akiwa na beji ya unahodha wa klabu hiyo lakini ilikuwa ni kama nuksi kwake kwani ndilo lilikuwa tamasha la mwisho kwake kushiriki sio tu akiwa kama nahodha bali pia mchezaji wa klabu hiyo.

JONAS MKUDE - 2016

Kijana aliyeibukia kikosi cha vijana cha Simba, kiungo Jonas Mukude naye alionja ladha ya kuiongoza Simba akiwa kama nahodha kwenye tamasha la Simba Day mwaka 2016 akirithi mikoba ya Nassoro Masoud ‘Chollo’.

Kama ilivyokuwa kwa Chollo, Mkude naye alishiriki tamasha hilo mara moja tu akiwa nahodha kwani baada ya hapo alivuliwa jukumu hilo.

METHOD MWANJALE - 2017

Mzimbabwe Method Mwanjale ni raia wa pili wa kigeni kushiriki Tamasha la Simba Day akiwa nahodha mwaka 2017 akiachiwa beji na Mkude ambaye aliondolewa kwenye nafasi hiyo na benchi la ufundi la Simba. Mwanjalee hakudumu. Alitemwa dirisha dogo la usajili nafasi yake ilichukuliwa na Bocco.