Himid Mao uso kwa uso Ismaily leo

Dar es Salaam. Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Himid Mao leo atakiongoza kikosi chake cha Petrojet SC dhidi ya Ismaily katika mchezo wa Ligi Kuu Misri.

Kocha wa Petrojet SC, Tarek Yehia aliyechukua mikoba ya Hassan Shehata amempa Mao jukumu la kutibua mpigo ya timu pinzani  akishirikiana na Ahmed El Agouz.

Katika mchezo wake wa kwanza wa kufungua msimu waliocheza Julai 31 dhidi ya Zamalek, Himid alicheza kwa dakika zote tisini huku akionyeshwa kadi ya njano ndani ya dakika za nyongeza baada ya 90 kumalizika.

Himid aliipata kadi hiyo kwenye utekelezaji wa majukumu ya kuharibu mipango ya Zamalek ambao kabla ya mchezo huo, rekodi zilikuwa zikiwabeba kupata matokeo ya ushindi.

Hata hivyo, hadi mchezo huo unamalizika, timu hizo zilitoka suluhu. Katika mwendelezo wa michezo ya Ligi Kuu Misri leo, Himid atakuwa na kibarua kingine cha kuharibu mipango ya Ismaily.

Akiyazungumzia majukumu yake hayo mapya, Himid alisema huwa anafurahia zaidi uwanjani kucheza nafasi hiyo ambayo muda mwingine hutakiwa kuanzisha mashambulizi mbali na kukaba.

Mara baada ya mchezo wa leo, Himid ataiongoza tena Petrojet Ijumaa kwa kucheza ugenini dhidi ya Wadi Degla.